Na Helena Magabe Tarime.
Kampuni ya uwekezaji ya HAIPPA PLC, yenye makao yake makuu mjini Musoma, imezindua rasmi programu mpya ya uwekezaji iitwayo SMATIKA – Toleo Na.1, ikiwa ni mkakati wa kuwajengea Watanzania uwezo wa kushiriki moja kwa moja kwenye fursa kubwa za kiuchumi na kibiashara zinazopatikana ndani na nje ya nchi.
Akizungumza na Jambo TV, Mkurugenzi Mkuu wa HAIPPA PLC, Boniphace Ndengo, amesema SMATIKA ni programu ya ubunifu wa kampuni hiyo ambayo ilianza kutekelezwa Julai 1, 2025, na inalenga kutoa fursa kwa kila Mtanzania kushiriki katika mifumo rasmi ya uwekezaji, ikiwemo watoto chini ya miaka 18 kupitia wazazi na walezi wao.
“SMATIKA si tu akaunti ya uwekezaji, bali ni jukwaa la kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja kupitia elimu, masoko, ajira na huduma za kifedha,” amesema Ndengo.
Ajenda Tano Kuu za SMATIKA
Programu ya SMATIKA inaendeshwa chini ya ajenda tano ambazo zinabeba maono ya HAIPPA PLC pamoja na dira ya maendeleo ya taifa. Ajenda hizo ni:
- Kila Mtanzania awe na akaunti ya uwekezaji inayosimamiwa na HAIPPA PLC.
- Kila Mtanzania awe na hisa angalau 1,000 ndani ya HAIPPA PLC ili kushiriki katika maamuzi na mapato.
- Kila Mtanzania apate G-Card ambayo humwezesha kurejeshewa sehemu ya matumizi yake anaponunua bidhaa au huduma.
- Kila Mtanzania apate elimu ya fedha na uwekezaji ili kufanya maamuzi ya kisera na kiuchumi kwa uelewa mpana.
- Kila Mtanzania ashikilie fursa katika miradi mikubwa, sekta za kimkakati na kutumia jukwaa la HAIPPA Afrika kutangaza na kuuza bidhaa na huduma zake kwa njia ya ubunifu na teknolojia.
Ndengo ameongeza kuwa SMATIKA ni mfumo hai utakaoboreshwa kadri mahitaji ya wananchi yanavyojitokeza na utaendeshwa kwa kuzingatia misingi ya kibiashara huku ushiriki ukiwa wa hiari.
“Tunataka Watanzania waone kuwa kushiriki kwenye uwekezaji si jambo la watu wachache au wenye mitaji mikubwa tu – bali kila mmoja ana nafasi,” alisema.
HAIPPA PLC pia imedhamiria kuendelea kutoa matoleo ya taarifa kwa umma kuhusu maendeleo ya programu hiyo, fursa mpya za uwekezaji, na namna Watanzania wanavyoweza kushiriki kikamilifu kwenye ukuaji wa uchumi wa taifa.