Na Helena Magabe-Tarime.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdalla, amemkabidhi tuzo maalum Nyambari Nyangwine kutokana na mchango wake mkubwa katika kuendeleza na kueneza lugha ya Kiswahili kupitia kazi za uandishi na uchapishaji wa vitabu.
Tuzo hiyo imetolewa na Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) kwa kushirikiana na Baraza la Kiswahili Zanzibar (BAKIZA) kama sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani ambayo mwaka huu yamefikia mwaka wa nne tangu kuanzishwa kwake na UNESCO.
Nyangwine, ambaye ni miongoni mwa wafanyabiashara wakubwa nchini na pia mwandishi mashuhuri wa vitabu vya Kiswahili, ametambuliwa kwa mchango wake wa kipekee katika kukuza maarifa kwa njia ya maandiko na kuhamasisha matumizi ya Kiswahili fasaha katika jamii.
Mbali na uandishi wake, Nyangwine aliwahi kuwa Mbunge wa Tarime kati ya mwaka 2010 na 2015. Kwa sasa ameshatangaza nia ya kugombea ubunge wa Jimbo la Tarime Vijijini kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025.
Kupokelewa kwa tuzo hiyo kumewasha ari mpya miongoni mwa wafuasi na jamii inayomzunguka, huku wengi wakieleza kuwa hatua hiyo imezidi kuongeza heshima ya Nyangwine kitaifa na kimataifa.
Tuzo ya Kiswahili ni moja kati ya nyenzo muhimu zinazotumika kutambua wadau wanaojitolea katika kukuza lugha hiyo, hasa kipindi hiki ambapo Kiswahili kinazidi kupata hadhi ya kimataifa, kikifundishwa katika vyuo vikuu duniani kote na kutumika kama lugha rasmi ya kidiplomasia na biashara Afrika Mashariki na Kati.