Latest Posts

TAKUKURU YATAKA VIONGOZI WA DINI WASIMAMIE MAADILI YA UCHAGUZI

Viongozi wa dini, wazee wa mila na asasi za kiraia wametakiwa kushirikiana kwa karibu katika kupambana na vitendo vya rushwa wakati huu taifa likielekea kwenye uchaguzi mkuu, ili kusaidia jamii kupata viongozi bora, waadilifu na wenye kuzingatia masuala ya haki, uongozi na maendeleo ya wananchi.

Wito huo umetolewa na Naibu Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Katavi, Stewart Kiondo, alipokuwa akifungua semina ya mafunzo kwa wadau hao, iliyofanyika mkoani Katavi kwa lengo la kuwajengea uwezo juu ya nafasi yao katika mapambano dhidi ya rushwa kipindi cha uchaguzi.

Kiondo amesema kuwa Ibara ya 9(h) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaelekeza mamlaka na taasisi zote kuhakikisha zinachukua hatua madhubuti za kutokomeza rushwa, jambo ambalo limepewa nguvu pia na Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Sura ya 329, hasa kupitia Kifungu cha 7(b) na Kifungu cha 15, vinavyolitaka TAKUKURU kuhamasisha ushiriki wa wananchi na taasisi nyingine katika mapambano hayo.

Amesisitiza kuwa viongozi wa dini wanapaswa kutumia busara na hekima kukemea vitendo vya wagombea wanaojipatia umaarufu kupitia ahadi za miundombinu au misaada ya kifedha, jambo ambalo ni mwanya wa rushwa ya uchaguzi.

Aidha, ameonya juu ya tabia ya baadhi ya wananchi kuwa na kauli kama “unatuachaje?” pindi wagombea wanapokuwa tayari wamepita au kuchaguliwa, akieleza kuwa hiyo ni sehemu ya kushabikia rushwa na kuharibu misingi ya uchaguzi huru na wa haki.

Kwa upande wake, Shehe Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Nassoro Kakulukulu, akizungumza kwa niaba ya washiriki wa semina hiyo, amesema mafunzo hayo yametoa mwanga mpya kuhusu wajibu wa viongozi wa kijamii katika kulinda maadili ya uchaguzi.

Amesema ni wajibu wao sasa kuwahimiza waumini wao kutambua thamani ya kura yao na madhara ya kuchagua viongozi kwa misingi ya rushwa, kwani wagombea hao huingia madarakani wakiwa na lengo la kufidia kile walichotoa.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!