Latest Posts

ACT YAVUTANA SHATI NA POLISI KUHUSU ULINZI WA KURA UCHAGUZI MKUU

Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Bara, Isihaka Mchinjita, ameonesha kushangazwa na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, kwa kauli yake ya kupinga raia kushiriki katika ulinzi wa kura wakati wa uchaguzi, akidai kuwa ni kinyume cha mantiki ya haki za kiraia na mchakato wa kidemokrasia.

Kupitia chapisho lake katika mtandao wa X (zamani Twitter), Mchinjita ameandika: “Ulinzi na usalama ni jukumu la kila raia. Jeshi la Polisi kujitokeza hadharani kukataa raia kushiriki ulinzi wa kura katikati ya tuhuma za polisi kushiriki wizi wa kura na kushindwa kuwachukulia hatua wezi wa kura waliofikishwa mikononi mwa polisi ni wazo la kihalifu.”

Kauli hiyo imekuja saa chache baada ya Kamanda Muliro kuhojiwa na Clouds TV, ambapo alihoji mantiki ya baadhi ya watu kutaka kulinda kura ilhali vyama tayari vina mawakala. Katika mahojiano hayo, Muliro alieleza kuwa shughuli ya ulinzi wa kura ni ya kisheria na inapaswa kufanywa na mamlaka husika pekee, si kila raia.

“Sasa ukisema unalinda mimi nakuuliza unalindaje? Ukisema unalinda hivi, mimi naangalia sharia, unalinda kwa kulala kwenye boksi la wapiga kura, unalinda kwa kukaa ndani kwa wapiga kura, unalindaje? kwa mamlaka yapi ya kisheria? Mimi sibishani lakini naiuliza sharia, yaani kila unachosema mimi naiuliza sheria, sheria inasema nini kuhusu jambo unalolisema maana yake mambo haya ya uchaguzi ni mambo makubwa, huwezi ukayaacha yakaenda bila utaratibu, tufanye kila mtu analinda, watu watahesabu vipi? Kama unalinda, wawakilishi wa nini sasa?”, alisema Muliro.

Hata hivyo, ACT Wazalendo imekuwa mstari wa mbele kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika kulinda mchakato wa uchaguzi, ikiwa ni pamoja na kuhamasisha wananchi kulinda kura zao baada ya kupiga kura kupitia kampeni yao ya kitaifa ya “Oktoba Linda Kura”.

Kwa mujibu wa Mchinjita, historia ya chaguzi za nyuma imeonesha kuwa baadhi ya maafisa wa usalama wamehusishwa na wizi wa kura na kuwazuia wananchi waliokuwa wakitaka kufuatilia matokeo katika maeneo mbalimbali ya nchi. Amesema hali hiyo imezua mashaka kwa wananchi kuhusu uaminifu wa vyombo vya dola katika kusimamia haki za kidemokrasia.

“Raia wana haki ya kujua hatima ya kura zao. Usimamizi wa kura hauwezi kuwa wa mtu mmoja au taasisi moja. Ni lazima kila mwananchi awajibike kuhakikisha kura yake haipotei,” ameongeza Mchinjita.

ACT Wazalendo imesisitiza kuwa ulinzi wa kura siyo uchochezi, bali ni namna ya kuwahamasisha wananchi kuwa na umiliki wa mchakato wa kidemokrasia na kulinda haki yao ya kikatiba ya kuchagua viongozi wanaowataka.

Uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025 unakaribia huku mvutano ukiendelea kati ya serikali na vyama vya upinzani kuhusu mazingira ya uchaguzi, sheria, na wajibu wa vyombo vya usimamizi.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!