Walengwa wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii nchini (TASAF) wameiomba serikali kuendelea kuwekeza katika mfuko huo ili kusaidia wananchi wengi zaidi kuondokana na umasikini na kujitegemea kiuchumi.
Ombi hilo limetolewa na Pili Selemani, mmoja wa wanufaika wa mpango huo, alipokuwa akizungumza kwenye Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo (Nanenane) yanayoendelea katika viwanja vya Nzuguni, jijini Dodoma.
Selemani amesema TASAF imekuwa mkombozi mkubwa kwa jamii zenye kipato cha chini, ambapo kupitia mpango huo, kaya nyingi zimeweza kupata milo mitatu kwa siku na kuanzisha shughuli ndogondogo za ujasiriamali.
“Tunaiomba serikali iendelee kuwekeza katika mfuko wa TASAF kwa kuwa umetusaidia sana. Kupitia fedha tunazopokea, tumeweza kujikimu na kusaidia familia zetu,” amesema Pili.
Akisimulia mafanikio aliyoyapata, Selemani amesema awali alikuwa hana uhakika wa kupata chakula, lakini sasa ameweza kuanzisha biashara ndogondogo inayomuwezesha kusomesha watoto wake na kumudu mahitaji ya msingi ya familia.
Naye Mariam Kassim, ambaye pia ni mnufaika wa TASAF, amesema mfuko huo umemwezesha kutoka kwenye lindi la umasikini na kuanzisha miradi ya ujasiriamali inayompatia kipato cha kila siku.
“Kupitia TASAF nimeweza kutengeneza bidhaa mbalimbali za matumizi ya nyumbani. Nawaalika wananchi wajitokeze kwenye maonyesho ya Nanenane ili wajifunze namna ya kujiinua kiuchumi kupitia ujasiriamali,”Amesema Mariam.
Aidha, amesema serikali aingalie uwezekano wa kuwapatia walengwa vitendea kazi, ili kuongeza ufanisi katika shughuli zao za kiuchumi na kuwafanya waweze kujitegemea zaidi.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa TASAF, Melkizedek Nduye, amewataka wananchi kutembelea banda la TASAF ili kujifunza zaidi kuhusu namna mfuko huo unavyofanya kazi na jinsi walengwa wanavyotumia misaada ya kifedha kuanzisha miradi ya maendeleo.
“Mbali na kuwapatia fedha walengwa, TASAF pia hutoa elimu kuhusu matumizi sahihi ya fedha hizo, ikiwa ni pamoja na namna ya kuanzisha na kuendeleza biashara ndogo ndogo,” amesema Nduye.
Ameongeza kuwa lengo kuu la TASAF ni kuhakikisha walengwa wanajitegemea kwa muda mrefu kupitia ujasiriamali na shughuli za uzalishaji, hata baada ya kumaliza kipindi cha kupokea ruzuku kutoka kwa mfuko huo.
Maonesho ya Nanenane yamekusanya wakulima, wajasiriamali, na wadau mbalimbali wa maendeleo kutoka mikoa yote ya Tanzania, yakiwa na kaulimbiu inayolenga kuinua kilimo, ufugaji na ujasiriamali wa kijamii na kiuchumi.