Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Katavi imeendesha mafunzo maalum kwa makundi mbalimbali ya kijamii kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya rushwa kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba.
Mafunzo hayo yaliyofanyika siku ya Ijumaa katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Katavi yalihusisha viongozi wa bodaboda na bajaji, watendaji kata, walimu wa klabu za kupinga rushwa na wafanyabiashara.
Mshiriki wa mafunzo hayo ambaye pia ni mwakilishi wa wafanyabiashara mjini Mpanda, Aman Mahella, amesisitiza kuwa mikopo inayotolewa karibu na kipindi cha uchaguzi imekuwa ikiambatana na ujumbe wa kisiasa unaoashiria vitendo vya rushwa.
“Mnafikiri kwanini vijana na wanawake wanapata mikopo karibu na uchaguzi? Ujumbe unaoambatana na mikopo sio mzuri,” amesema Mahella akisisitiza suala hilo lichunguzwe kwa kina na TAKUKURU.
Kwa upande wake, Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Katavi, Sipha Mwanjala, amebainisha kuwa rushwa ni tishio kwa msingi wa demokrasia na haikubaliki katika jamii. Amesisitiza kuwa taasisi yake haitarudi nyuma katika mapambano dhidi ya rushwa hadi pale vitendo hivyo vitakapokoma.
“Rushwa si kwamba tu inapotosha mwelekeo wa uamuzi kwa wananchi bali pia inapunguza imani ya wananchi kwa vyombo vya uchaguzi na serikali kwa ujumla,” amesema Mwanjala.
Awali, akifungua mafunzo hayo, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Katavi, Florence Chrisant, amefananisha rushwa na tendo la mauaji linalopaswa kupigwa vita kwa nguvu zote na jamii.
Amesema washiriki wa mafunzo hayo wanapaswa kuwa mabalozi wa kutoa elimu ya madhara ya rushwa na kuhakikisha jamii inashirikiana kudhibiti vitendo hivyo kwa ustawi wa taifa.