Sheikh Mkuu Mkoa wa Mwanza, Hassan Kabeke ameitaka Ofisi Kuu ya Shughuli za Hijja Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (Biitha) kwenda kushughulikia tuhuma za uongo zinazoenezwa na baadhi ya watu kuhusu Ibada ya Hijja huku akiwataka kuja na majibu.
Akizungumza Jijini Mwanza kwenye Kongamano Maalumu la uhamasishaji wa Ibada ya Hijja 2026, Sheikh Kabeke amesema baadhi ya waumini wa dini hiyo wamekuwa wakiwaaminisha wenzao na kuwatisha kuwa wanaoenda kushiriki ibada ya Hijja hufariki mapema jambo ambalo sio kweli.
“Yako mambo ya uongo wanayosema juu ya Hijja mimi nadhani Biitha iwe na kazi ya kuyaorodhesha na kuyapatia majibu, yupo mtu anaambiwa usiende Hijja ukienda, ukirudi unakufa,” amesema.
Akiunga mkono hoja hiyo Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Amir Mkalipa amesema vijana wengi hawajaandaliwa kikamilifu namna ya kutafuta fedha itakayo wawezesha kushiriki ibada ya Hijja hivyo kuwata Masheikh kuwekeza pia elimu kwa vijana juu ya namna ya kutafuta fedha.
Rais wa Biitha Tanzania, Sheikh Abdulla Talib Abdalla ameeleza shauku yake kubwa kuwa ni kuona waumini wa dini hiyo kutoka mkoani Mwanza kuanza kufanya maandalizi ya kushiriki ibada hiyo mwaka 2026.
Kwa upande wake Imamu wa Msikiti wa Mtoro uliopo Dar es Salaam, Othmani Khamissi amedai watu wote wanao uwezo wa kushiriki ibada ya Hijja lakini kinacho wakwamisha ni kutofuata utaratibu uliowekwa na Mwenyezi Mungu.