Chama cha Waganga wa Tiba Asili na Tiba Mbadala Tanzania (TAMESOT) kimepinga vikali mauaji ya mwanafunzi wa kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Qash, wilayani Babati mkoani Manyara, yaliyosababishwa na ramli chonganishi.
Tukio hilo lililotokea tarehe 16 Agosti 2025 saa 11 alfajiri katika kijiji cha Qash, limesababisha kifo cha mwanafunzi Yohana Atanas Konk, baada ya wenzake kumshambulia wakimtuhumu kuiba simu kubwa ya “tach”. Inadaiwa wanafunzi hao walichochewa na maneno ya mganga wa tiba asili anayejiita Abduli Mustafa (maarufu Osters), ambaye alitaja jina la marehemu kupitia ramli chonganishi.
Taarifa ya TAMESOT iliyotolewa, Agosti 18, 2025 na Katibu Mkuu wa chama hicho, Lukas Joseph Mlipu, imeeleza kuwa taarifa za tukio hilo ziliwasilishwa kwao na mwenyekiti wa kijiji cha Qash, Sosi Abdalah Sosi, na wamepokea kwa masikitiko makubwa habari za kifo cha kijana huyo.
“TAMESOT tunalaani vikali tukio hili na tunapongeza Jeshi la Polisi kwa hatua ya kuwatia nguvuni wanafunzi waliohusika. Tunaamini baada ya uchunguzi hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wote waliokatisha maisha na ndoto za mwanafunzi huyu,” amesema Mlipu.
Aidha, chama hicho kimewataka waganga wa tiba asili kote nchini kuzingatia kanuni na miongozo ya kisheria katika utoaji huduma zao, na kuonya wale wanaotumia ramli chonganishi zinazosababisha madhara katika jamii.
“Tunaendelea kuwasihi waganga wa tiba asili kujiunga na chama chetu ili kupata elimu itakayowaongoza vyema katika majukumu yao ya utoaji huduma kwa jamii,” iliongeza taarifa hiyo.
TAMESOT pia kimeeleza pole kwa wazazi wa marehemu, walimu, wanafunzi wa Shule ya Sekondari Qash, jamii ya kijiji cha Qash na Tsamasi pamoja na Serikali, kwa kumpoteza kijana ambaye ulikuwa ni miongoni mwa nguvukazi ya taifa la kesho.