Latest Posts

POLISI PWANI: WALIOKAMATWA SIO MAKADA WA CHADEMA, NI WAHALIFU

Mvutano umeibuka kati ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani kufuatia kukamatwa kwa watu 10 wanaodaiwa kuwa wanachama wa chama hicho katika kikao cha ndani kilichodaiwa kufanyika Kibaha, Agosti 16, 2025.

Kwa mujibu wa taarifa ya CHADEMA, kati ya waliokamatwa ni Pendo Msechu, Pendo Kyosi, Mary Mushi, Samson Mzambia, Focus Laurent na Alfred Bundala, ambao walihamishiwa Kituo Kikuu cha Polisi (Central) jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo, Agosti 17 Jeshi la Polisi mkoani Pwani lilieleza kuwa watu hao walikamatwa si kwa sababu ya shughuli za kisiasa bali kwa tuhuma za kupanga njama za kutenda uhalifu katika ukumbi wa Mwitiongo, Maili Moja Kibaha.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Salim Morcase, alisema watuhumiwa hao wanaendelea kuhojiwa na upelelezi ukikamilika hatua za kisheria zitachukuliwa.

Lakini kupitia taarifa iliyotolewa Agosti 19 na Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa CHADEMA, Brenda Rupia, chama hicho kilieleza kusikitishwa na hatua ya polisi kuendelea kuwatia nguvuni wanachama wake 10 bila kuwapatia haki ya kuonana na mawakili wao, ndugu, wala kufikishwa mahakamani.

“Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kinasikitishwa na kitendo cha Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani kuendelea kuwashikilia wanachama 10 bila kuwapatia haki ya kuonana na mawakili wao na au kuwafahamisha ndugu zao” imesomeka sehemu ya taarifa hiyo.

CHADEMA imeitaka polisi kutoa ushirikiano kwa ndugu na mawakili, pamoja na kutoa taarifa rasmi juu ya walipo na hatua za kisheria zinazofuata.

Akijibu hoja hizo kwa mujibu wa tovuti ya Mwananchi, Morcase amesema: “Waulize wao (CHADEMA) walikutana na nani? Maana mimi sijakamata mtu wa CHADEMA. Nimekamata wahalifu sawa brother (kaka), hiyo ya CHADEMA waambie wakamuulize mtu anayehusika na vyama vya siasa”.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!