Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Prof. Palamagamba Kabudi, amewataka viongozi wa kisiasa kutumia vyombo vya habari ipasavyo kwa ajili ya kunadi sera na mipango ya vyama vyao badala ya kuwashambulia au kuwachambua watu binafsi.
Akitoa hotuba yake, Agosti 21, 2025, katika Mkutano wa Wadau wa Habari na Utangazaji Kanda ya Mashariki uliofanyika katika ukumbi wa PSSSF mkoani Dar es Salaam, Waziri Kabudi amesema vyombo vya habari ni nyenzo muhimu za kuwahamasisha wananchi kushiriki uchaguzi kupitia mijadala ya redio, televisheni na mitandao ya kijamii.
Amesema matumizi bora ya vyombo vya habari huchangia kuongeza uelewa wa kisiasa kwa wananchi na kuimarisha demokrasia nchini. Aidha, amesisitiza umuhimu wa kila Mtanzania kulinda amani na kuepuka kutanguliza maslahi binafsi badala ya uzalendo kwa maendeleo ya taifa.
“Ndugu zangu, nchi hii ni yetu sote na hatuna nchi nyingine zaidi ya nchi hii iitwayo Tanzania. Hii ndiyo mashua yetu, hii ndiyo meli yetu, tusiruhusu hata mara moja mashua hii au meli hii izame au ipate dhoruba na kuharibika,” amesema Kabudi.
Prof. Kabudi amewakumbusha Watanzania kuwa waasisi wa taifa walilipigania kwa gharama kubwa, hivyo ni wajibu wa kila mmoja kulilinda na kudumisha amani ili taifa liendelee kustawi.