Latest Posts

TCRA, POLISI WAVITAKA VYOMBO VYA HABARI KUKEMEA VURUGU UCHAGUZI 2025

Meneja wa Huduma za Utangazaji kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Mhandisi Andrew Kisaka, amewataka waandishi wa habari kuwa mstari wa mbele kukemea vurugu na migogoro yoyote itakayojitokeza wakati wa Uchaguzi Mkuu wa 2025 badala ya kushiriki kwa njia ya kuripoti au kuchochea.

Akizungumza Agosti 21, 2025 katika mkutano wa wadau wa sekta ya habari na utangazaji Kanda ya Mashariki uliofanyika mkoani Dar es Salaam, Kisaka amesema waandishi wanapaswa kutanguliza utu na kuelimisha jamii ili kuepusha umwagaji damu, hotuba za chuki na matendo ya kikatili.

“Tukemee vurugu kila mara zinapojitokeza, maneno ya viongozi na hata wananchi wa kawaida yanaweza kuzuia machafuko. Vyombo vya habari vinapaswa kurudia kwa nguvu kulaani aina zote za vurugu dhidi ya raia na mali zao, huku vikihakikisha vinarejesha utu wa Mtanzania,” amesema Kisaka.

Ametoa onyo kwa vyombo vya habari vya mtandaoni (online media) vinavyotumia vichwa vya habari vya kuchochea migogoro na kudhalilisha, akivitaka kuzingatia umakini katika kuchapisha habari na kuepuka kueneza taarifa zisizo sahihi.

Kwa upande wake, Msemaji Mkuu wa Jeshi la Polisi, DCP David Misime, amesema waandishi wana jukumu la kuelimisha umma kuhusu sheria, maadili, haki na wajibu wakati wa uchaguzi na kuepusha kusambaza taarifa za uongo na uchochezi.

“Kuhakikisha mchakato wa uchaguzi unafanyika katika hali ya amani, utulivu na usalama ndilo jukumu letu. Polisi watachukua hatua zote muhimu za usalama pale watakapoona dalili za uvunjifu wa amani,” amesema DCP Misime.

Aidha, amebainisha kuwa Jeshi la Polisi litahakikisha usalama wa wagombea, wapiga kura na vituo vya kupigia kura, huku akisisitiza mshikamano kati ya jamii na vyombo vya habari kwa ajili ya kulinda amani na haki za binadamu.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!