Wafanyabiashara wadogo na wa kati mkoani Iringa wameeleza kufaidika kwa kiasi kikubwa na maonyesho ya biashara yajulikanayo kama Iringa Business Connect, ambayo yamewasaidia kufungua fursa mbalimbali za kibiashara na kupata elimu muhimu kuhusu uboreshaji wa shughuli zao, ikiwemo namna ya kulipa kodi sahihi na kuepuka vikwazo vinavyokwamisha maendeleo ya biashara zao.
Wakizungumza wakati wa kufunga rasmi maonyesho hayo, wafanyabiashara hao walieleza kuwa wamepata maarifa ya thamani kuhusu usajili wa biashara, umuhimu wa kuwa katika mfumo rasmi wa kodi, na matumizi ya teknolojia katika uendeshaji wa biashara.
Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoa wa Iringa na Mwenyekiti wa maonyesho hayo, Peter Jackson, alisema kuwa maonyesho ya mwaka huu yamekuwa ya mafanikio makubwa kwani zaidi ya wananchi elfu mbili wamepatiwa elimu mbalimbali ya namna ya kufanya biashara zao kwa lengo lakujikwamua kiuchumi
Aliongeza kuwa TRA inaendelea kuimarisha huduma zake kupitia mifumo ya kidigitali, ili kuwawezesha wananchi kupata huduma kwa urahisi, haraka, na kwa ufanisi mkubwa.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Benjamin Sitta, alihitimisha kongamano hilo kwa kutoa wito kwa waandaaji kuhakikisha kuwa maonyesho hayo yanakuwa endelevu kila mwaka.
Alisisitiza kuwa maonyesho kama hayo ni fursa adhimu kwa vijana na wanawake kujifunza, kujiajiri, na kukuza uchumi wao kupitia maarifa wanayoyapata.
Kongamano hilo liliandaliwa kwa lengo la kuwawezesha wananchi, hususan wafanyabiashara wadogo na wa kati pamoja na wajasiriamali, kuingia katika mfumo rasmi wa biashara kwa kusajili biashara zao, kupata Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN), na kutumia huduma za kidigitali zinazotolewa na TRA.