Latest Posts

CHADEMA YATAKA UKAGUZI WA KIMATAIFA WA MIFUMO YA UCHAGUZI

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Bara, John Heche, amesema chama chake kiko tayari kuchukua hatua za kusafisha mifumo ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) ambayo inadaiwa kuunganishwa na mifumo mingine mikubwa ya taifa, ikiwemo Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Akizungumza Agosti 27, 2025 kupitia Baraza la Kidigitali la CHADEMA kwa njia ya mtandao, Heche amesema CHADEMA imeandaa hatua mahsusi kuhakikisha haki na uwazi katika uchaguzi ujao.

Miongoni mwa hatua alizozitaja ni kuandika barua kwa taasisi za kimataifa kuomba wakaguzi wa uchaguzi wa kimataifa kuikagua mifumo ya uchaguzi ya Tanzania na kuweka matokeo wazi kwa wananchi, kuomba Mahakama ya Afrika Mashariki kuishinikiza Tanzania kuruhusu ukaguzi huru wa mifumo ya uchaguzi na kuwajulisha wakuu wa majeshi nchini kuhusu hali hiyo kwa madai kuwa “mifumo ya taifa imeingiliwa.”

Vuguvugu hili limeibuka kufuatia kauli ya kada wa CCM, Humphrey Polepole, aliyedai mifumo ya uchaguzi, NIDA na CCM kuwa imeunganishwa, jambo ambalo viongozi wa CHADEMA wanasema walishalalamikia kwa muda mrefu.

Aidha, CHADEMA imewaomba viongozi wa dini nchini kuwaelekeza waumini wao kutoshiriki uchaguzi endapo mifumo hiyo haitakaguliwa, wakisisitiza kuwa mapambano ya kulinda demokrasia si jukumu la chama pekee bali la wananchi wote.

“Wananchi lazima waelewe hakuna aliye salama. Ni wajibu wa kila mmoja kusimama na kupigania heshima ya kura yake. Nguvu ya umma ndiyo italeta mabadiliko,” ameongeza Heche.

Hata hivyo kauli hiyo ya Polepole juu ya mifumo ya uchaguzi ililazimu wakuu wa taasisi husika kujitokeza hadharani na kukanusha.

Mkurugenzi Mkuu wa NIDA, James Kaji, alisema madai hayo “hayana ukweli wowote,” huku akisisitiza hakuna mfumo wa NIDA uliowahi kufungamanishwa na chama cha siasa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa INEC, Ramadhan Kailima, kupitia taarifa ya Agosti 23, 2025, alikanusha kuwa mifumo ya uchaguzi imeunganishwa na NIDA au chama chochote cha siasa.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!