Latest Posts

UJENZI WA VYOO SHULE YA MSINGI KILOLELI WAPUNGUZA UTORO, WAIMARISHA USALAMA WA WANAFUNZI

Sikonge, Tabora

Wananchi wa Wilaya ya Sikonge mkoani Tabora wameeleza kufurahishwa na utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa matundu 10 ya vyoo katika Shule ya Msingi Kiloleli, unaotekelezwa kupitia ufadhili wa Shirika la Kuhudumia Watoto Dunianiani @uniceftz na Serikali ya Canada @canada_embassy_tz chini ya usimamizi wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) wenye thamani ya takribani milioni 30.

Mradi huo, ambao umelenga kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia, umeleta matumaini mapya kwa jamii ya eneo hilo, hususan wazazi na wanafunzi waliokuwa wakikabiliwa na changamoto kubwa ya miundombinu ya vyoo shuleni hapo.

Akizungumza wakati wa ziara ya timu kutoka TEA, Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Mwl. Festo Ponela, alisema shule hiyo iliyoanzishwa mwaka 1974 ina jumla ya wanafunzi 831, lakini kwa muda mrefu ilikuwa na matundu sita tu ya vyoo.

“Shule yetu ilikuwa na matundu sita tu ya vyoo kwa wanafunzi 831. Hali hiyo ilisababisha changamoto kubwa ya msongamano na hata kuhatarisha usalama wa watoto. Pia ilichangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la utoro miongoni mwa wanafunzi,” alisema Mwl. Ponela.

Kwa upande wake, Bi. Rehema Usega, ambaye alizungumza kwa niaba ya wazazi wa wanafunzi wa shule hiyo, alisema ujio wa mradi huo umeleta mabadiliko makubwa, kwani watoto sasa wanasoma katika mazingira bora zaidi.

“Awali watoto walikuwa wakikosa masomo kabisa kutokana na changamoto ya vyoo. Kwa sasa wazazi tuna amani, watoto wanahudhuria masomo kwa wakati na utoro umepungua kwa kiasi kikubwa. Tunashukuru sana kwa mradi huu,” alisema Bi. Usega.

Mradi huu ni sehemu ya juhudi za TEA kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo, kuhakikisha shule za msingi na sekondari nchini zinakuwa na miundombinu bora inayowezesha utoaji wa elimu salama, jumuishi na yenye tija kwa watoto wote wa Kitanzania.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!