Latest Posts

TEF YAMLILIA DANIEL MBEGA, IKIKUMBUKA MCHANGO WAKE KATIKA KUKUZA TASNIA YA HABARI NCHINI

 

Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) limethibitisha kufariki kwa mwanachama wake, Daniel Mbega, ambaye alikuwa mmoja wa waandishi wa habari mahiri nchini, leo Jumamosi, Oktoba 11, 2025, katika Hospitali ya Temeke, jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na familia, marehemu Mbega alizidiwa ghafla majira ya saa 10 alfajiri na alikimbizwa Hospitali ya Temeke kwa matibabu. Hata hivyo, juhudi za madaktari kumwokoa hazikuzaa matunda, na alifariki dunia wakati akiendelea kupatiwa huduma.

Mbega alikuwa mwandishi wa habari mwenye uzoefu wa zaidi ya miongo miwili, akibobea katika uandishi wa habari za uchunguzi (investigative journalism).

Katika kipindi cha taaluma yake, amefanya kazi na vyombo kadhaa vya habari nchini na kuchangia kwa kiasi kikubwa kukuza weledi, uwajibikaji, na maadili ya taaluma ya habari Tanzania.

Alipata elimu yake ya msingi katika Shule ya Msingi Chigwingwili wilayani Kongwa, mkoa wa Dodoma, kabla ya kuendelea na masomo ya sekondari katika Shule ya Sekondari Pugu. Baadaye alisomea uandishi wa habari katika Tanzania School of Journalism (TSJ), ambako alianza kujenga msingi wa taaluma iliyomtambulisha hadi kifo chake.

Hadi umauti unamfika, Mbega alikuwa mwanachama hai wa TEF, akitambulika kwa mchango wake wa kitaaluma, nidhamu, na kujitolea katika juhudi za kutetea uhuru wa vyombo vya habari nchini.

Kwa mujibu wa taarifa ya TEF, mwili wa marehemu utaagwa kesho, Jumapili Oktoba 12, 2025, katika Hospitali ya Temeke, kabla ya kusafirishwa kwenda kwao Chigwingwili, wilayani Kongwa, mkoani Dodoma, kwa maziko yanayotarajiwa kufanyika Jumatatu Oktoba 13, 2025.

“TEF inaungana na familia, ndugu, jamaa, marafiki na wanahabari wote nchini katika kipindi hiki kigumu. Tunatoa pole za dhati kwa familia ya marehemu na tunamuombea Mwenyezi Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi,” imeeleza sehemu ya taarifa iliyosainiwa na Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile, leo Oktoba 11, 2025.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!