Latest Posts

WATU 6 WAKAMATWA KWA KUHAMASISHA MAANDAMANO

Jeshi la Polisi Tanzania limekanusha taarifa zinazosambazwa mtandaoni zikidai kuwa watu saba wamekamatwa katika mazingira ya kutatanisha, likisema kuwa waliokamatwa walitiwa nguvuni kwa mujibu wa sheria kutokana na tuhuma za uhalifu, zikiwemo za uchochezi na kuhamasisha maandamano yasiyo halali.

Kupitia taarifa yake kwa umma iliyotolewa Oktoba 17, 2025, Makao Makuu ya Polisi Dodoma, kupitia Msemaji wake DCP David Misime, Jeshi hilo limesema, “Miongoni mwa watu sita waliotajwa katika taarifa hizo, walikamatwa kwa mujibu wa taratibu za kisheria kutokana na ushahidi uliokuwa umekusanywa kabla ya kukamatwa kuhusiana na tuhuma mbalimbali za kihalifu.”

Jeshi hilo limefafanua kuwa watuhumiwa hao walikamatwa kwa kosa la matumizi mabaya ya mitandao kwa kufanya uchochezi na kuhamasisha maandamano kinyume cha sheria.

“Wakati wa ukamataji watu walishuhudia na baadhi ya viongozi wao walifika katika ofisi za makamanda wa polisi mikoa na vituo vya polisi kuwaulizia, na walijulishwa kuwa watu sita wanashikiliwa na walielezwa tuhuma zao,” taarifa hiyo imeeleza.

Jeshi la Polisi limewataja waliokamatwa kuwa ni Chief Adronius Kalumuna, Paulo Shijason Musisi, Daniel Damian Lwebugisa, Egbert Aloyce Kikulega, Ramadhan Fadhiri na Baziri Waziri.

Aidha, Jeshi hilo limezungumzia pia taarifa zilizotolewa na mwanasiasa Godbless Lema kupitia mitandao ya kijamii akidai kuwa usalama wake upo hatarini, ambapo limesema linafuatilia kwa karibu suala hilo.

“Tunamsisitiza afike katika kituo cha polisi ili awasilishe taarifa yake rasmi kwa hatua zingine kwani ndiyo utaratibu wa kisheria,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Jeshi la Polisi limewataka viongozi na wananchi kuacha kutoa taarifa zisizo sahihi mitandaoni, likisisitiza umuhimu wa kufuata taratibu za kisheria kabla ya kuwasilisha taarifa kwa jamii.

“Tunaendelea kutoa wito na kusisitiza kwa baadhi ya viongozi na wananchi waendelee kuzingatia utaratibu wa kisheria wa kuwasilisha taarifa sahihi kwa jamii na mamlaka za haki jinai ili kuepusha upotoshaji na taharuki zisizo za lazima,” imeeleza taarifa hiyo iliyosainiwa na Msemaji wa Jeshi la Polisi, Makao Makuu, Dodoma.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!