Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Musalia Mudavadi ameitetea familia ya Rais William Ruto dhidi ya madai kwamba inanufaika kifedha kupitia mpango wa serikali wa kupeleka wafanyakazi wa nyumbani nchini Saudi Arabia.
Akihojiwa mbele ya Bunge la Kitaifa siku ya Jumatano, Mudavadi alikabiliana na maswali kuhusu taarifa ya New York Times iliyodai kuwa maafisa wa juu serikalini na hata familia ya Rais wanahusishwa na kunufaika na mfumo wa kuwasafirisha Wakenya wanaotafuta ajira katika nchi hizo, ambako wengi wanaripotiwa kukabiliwa na mazingira magumu.
Taarifa hiyo ilidai kuwa familia ya Rais Ruto ni miongoni mwa wamiliki wakubwa wa kampuni ya bima inayohusishwa na mchakato wa kupeleka wafanyakazi wa nyumbani nje ya nchi kwa gharama nafuu.
Taarifa iliyochapishwa na Citizen Digital imeripoti kuwa Mbunge wa Samburu Magharibi, Naisula Lesuuda, alimuuliza swali Mudavadi: “Bainisha iwapo kuna afisa yeyote mwandamizi serikalini anayemiliki kwa njia ya moja kwa moja au vinginevyo kampuni za uajiri, mafunzo au bima zinazohusika na kupeleka Wakenya katika nchi za Ghuba.”
Katika majibu yake, Mudavadi alikanusha vikali madai hayo, akisisitiza kuwa hakuna kampuni ya bima inayopatiwa ukiritimba wa kushughulikia Wakenya wanaotafuta ajira nje.
“Hatuhusiki na usafirishaji haramu wa binadamu, wala Rais au serikali yake hawahusiki na biashara ya utumwa,” alisema.
Aidha, aliongeza kuwa Bunge tayari limepitisha Muswada wa Mgongano wa Maslahi, na iwapo mtu yeyote atabainika kuwa na mgongano wa maslahi katika sekta hiyo, hatua stahiki zitachukuliwa.
Alifichua kuwa serikali ina orodha ya mashirika 594 ya uajiri, hivyo kuchunguza umiliki wa kila moja kunahitaji muda zaidi.