Vijana wa Tanzania wameeleza kufurahishwa na maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuanzisha Wizara ya Vijana, wakisema Waziri Joel Nanauka ni Kijana na wanaamini anazijua changamoto zote za Vijana.
Akizungumza siku chache mara baada ya kuapishwa kwa Baraza jipya la Mawaziri akiwemo Waziri Mhe. Joel Nanauka, Abua Magaira, Mkazi wa Dar Es Salaam ameeleza kumpokea kwa Mikono miwili waziri huyo, akisema dhamira ya Rais Samia ni kuona changamoto za Vijana zinashughulikiwa ipasavyo.
Abua amezungumzia pia dhamira ya Rais Samia ya kutafuta maridhiano kati ya wadau mbalimbali wa kisiasa na kijamii nchini, akiyataja kama maamuzi muhimu na ya kupongezwa kwani yatawezesha kuimarisha umoja na mshikamano wa Watanzania na makundi mbalimbali ya kijamii na kisiasa.
Katika hotuba yake ya kuzindua Bunge la 13, mwishoni mwa wiki iliyopita Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alisema kwa kuwa zaidi ya asilimia 60 ya watu nchini ni vijana hivyo Serikali itaweka kipaumbele kwenye sera na programu zitakazopanua fursa za kiuchumi, kutengeneza kazi na ajira, kuongeza wigo wa hifadhi za jamii, na kuwajengea kesho iliyo bora zaidi.
Alisema lengo ni kuhakikisha vijana wanapata nafasi ya kushiriki katika kujenga mustakabali mwema wa Taifa letu. “Tutaweka kipaumbele kwenye ushirikishwaji wa vijana katika masuala ya maendeleo yao. Natambua kumekuwa na majukwaa mengi ya kuwafikia vijana, ila bado shughuli zao zinafifishwa na masuala ya kisiasa, na majukwaa hayo kupoteza malengo na mvuto kwa vijana.