Na Amani Khamis Amani Mjege.
Wakati viongozi wa dunia walipokutana tarehe 14 Novemba 2025 huko Belém, Brazil, wakati wa Mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP30) kuidhinisha Azimio la Belém kuhusu Ukuaji wa Viwanda Endelevu vya Kijani Duniani, mjadala mkubwa ulimulika namna nchi zinavyoweza kuunganisha juhudi za kupunguza gesi joto na mageuzi ya kiuchumi kupitia viwanda vya kijani. Hata hivyo, Tanzania haimo miongoni mwa mataifa yaliyosaini azimio hilo kati ya nchi 35 na wadau wengine- swali likiwa: je, hii ni fursa iliyopotea au nafasi pana ya kutafakari kabla ya kujiunga?
Azimio hilo limetajwa na washirika hao kama hatua ya kihistoria ya kuunganisha ushirikiano wa kimataifa katika mageuzi ya viwanda na nishati, kuongeza uwekezaji, kuboresha teknolojia safi na kuhakikisha nchi zinazoendelea hazibaki nyuma. Shirika la Maendeleo ya Viwanda la Umoja wa Mataifa (UNIDO) na washirika wengine wanasema Belém inalenga “kuanzisha zama mpya za viwanda visivyochafua mazingira” ili kuharakisha kupunguza gesi joto duniani.
Gerd Müller, Mkurugenzi Mkuu wa UNIDO, alisisitiza kuwa Azimio la Belém linaunganisha malengo ya tabianchi na hatua halisi za maendeleo, ajira na teknolojia na kwamba ni nafasi muhimu kwa nchi zinazoendelea.”.

Kwa upande wa mwenyeji, Makamu wa Rais wa Brazil, Geraldo Alckmin, aliongeza kwamba azimio hilo linafungua milango ya ushindani mpya wa kiuchumi: “Kuendeleza viwanda vya kijani ni kuhusu kujenga viwanda na ajira za kesho.”
Lakini kwa nchi kama Tanzania ambayo imeweka malengo ya kupunguza gesi joto kwa asilimia 30–35 ifikapo 2030 swali la msingi ni namna ya kujiweka katikati ya mageuzi haya mapya.
Jambo TV imezungumza na mtaalamu wa mabadiliko ya tabianchi na uhifadhi wa mazingira, Baruani Mshale, ambaye anaamini kwamba Tanzania “haina cha kupoteza, bali inayo faida nyingi endapo itaamua kujiunga.”
“Nchi zilizotia saini zina nafasi ya kushirikiana kiteknolojia na kiuwekezaji. Tanzania ikiwa nje, tunaweza kukosa teknolojia safi tunazohitaji kwa viwanda na nishati,” amesema Mshale.
Anafafanua kuwa mataifa mengi yaliyojiunga tayari yanaongoza kwa teknolojia safi- kutoka nishati jadidifu, uchakataji wenye ufanisi, hadi viwanda visivyotoa hewa ukaa kwa kiwango kikubwa.

“Sasa hivi kwa mfano tunachimba na kuuza makaa ya mawe ambayo sio nishati safi. Tunachimba na kuuza hiyo natural gas ambayo na yenyewe kuna namna ambayo ambavyo inaweza ikafanywa kwa usafi zaidi ikawa ni shati safi, na kuna namna ambavyo inaweza ikafanyika ambayo sio safi…Kwa hiyo sisi tunaweza tukanufaika kwa kujiunga katika hii ambayo inasisitiza katika kupunguza athari hasi za hivyo viwanda vikubwa”, ameeleza.
Kwa maoni yake, kuendelea kusita kunaweza kuiweka Tanzania kwenye hatari ya kuzuiwa au kutozwa ushuru mkubwa iwapo itaamua kuendelea kuuza nishati au bidhaa zenye kiwango kikubwa cha uchafuzi, hasa makaa ya mawe na gesi isiyosafishwa, katika masoko ya nje yanayoenda kijani kwa kasi.
Mshale anasisitiza kuwa Tanzania inahitaji teknolojia za kusafisha uzalishaji wa viwanda, kubadilisha mifumo ya nishati na kuboresha ufanisi wa uzalishaji mambo ambayo yanahitaji ushirikiano wa kimataifa.

“tunazozihitaji hizo teknolojia katika hii ndoto yetu ya Tanzania ya viwanda tukielekea katika Tanzania ya uchumi tunaoutaka kama ilivyowekwa katika dira ya mwaka 2050. Kwa hiyo kwa kujiunga kwa kushirikiana na nchi ambazo wameridhia azimio hii tunajiweka katika nafasi ya kuweza kupata hizo fursa”, ameeleza.
Kwa mujibu wa Mshale, Tanzania inaweza kuwa mfano bora wa Afrika Mashariki endapo itaamua kujiunga baadaye. Anaamini Tanzania inaweza kubeba hadhi ya kuwa miongoni mwa mataifa ya mfano wa kuwa na viwanda safi kwa Afrika hasa ikiwa itachanganya uzalishaji wa umeme wa maji na jua, kuongeza uwekezaji wa haidrogeni, kuboresha miundombinu ya reli na kuondokana na mafuta mazito.
“Tutakuwa ni kiongozi katika maeneo hayo na tunaweza tukatengeneza uhusiano na ushirikiano na mashirika ya kimataifa, viwanda vikubwa duniani pamoja na nchi nyingine ambapo uhusiano huo unaweza ukawa na faida kwetu zaidi pale ambapo sisi tunakuwa tumeonesha kwamba kumbe inawezekana na sisi ni kinara katika kupelekea kufikia yale malengo ambayo dunia inatamani kuyafikia”, ameeleza.
Tanzania bado inategemea gesi na mabwawa ya maji, huku ikichimba makaa ya mawe kwa wingi. Azimio la Belém linafungua uwekezaji katika miradi mikubwa ya jua na upepo, mitambo ya kuchakata taka kuwa nishati, teknolojia za kupunguza hewa ukaa viwandani na kupata ufadhili wa kimataifa ili kutimiza malengo yake ya kitaifa ya kukubaliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.
Aidha, Tanzania ni miongoni mwa wachangiaji wadogo wa gesi joto duniani, lakini madhara ya mabadiliko ya tabianchi- ukame, mafuriko, na kuyumba kwa uzalishaji inakabiliwa nayo vikali. Azimio la Belém linaonekana kuwa jukwaa linaloweza kuisaidia taifa kupunguza gharama za mabadiliko huku ikipewa teknolojia, fedha na soko.