Latest Posts

NCHI 16 ZA MAGHARIBI ZATAKA UCHUNGUZI HURU MATUKIO YA OKTOBA 29 TANZANIA

Ubalozi wa Uingereza, Canada, Norway, Uswisi, Ubelgiji, Denmark, Ufini, Ufaransa, Ujerumani, Ireland, Italia, Uholanzi, Poland, Slovakia, Hispania, Uswidi, na Ujumbe wa Umoja wa Ulaya umetoa tamko zito likieleza “huzuni na wasiwasi mkubwa” kutokana na vifo, majeruhi na ukiukwaji wa haki za binadamu ulioripotiwa kutokea wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa Tanzania wa Oktoba 29, 2025, na kutaka uchunguzi huru, wazi na shirikishi.

Katika tamko lao la pamoja lililotolewa siku ya Ijumaa tarehe 5 Desemba 2025, nchi hizo zinazitaka mamlaka husika nchini kukabidhi miili ya waliopoteza maisha kwa familia zao “haraka iwezekanavyo”, kuwaachia huru wafungwa wote wa kisiasa, na kuhakikisha waliokamatwa wanapata msaada wa kisheria na matibabu.

“Taarifa za kuaminika kutoka mashirika ya kitaifa na kimataifa zinaonesha ushahidi wa mauaji nje ya utaratibu wa kisheria, kupotea kwa watu, ukamataji wa watu kiholela na ufichaji wa miili ya waliopoteza maisha. Tunatoa wito kwa mamlaka husika kukabidhi miili ya marehemu kwa familia zao haraka iwezekanavyo, kuwaachia huru wafungwa wote wa kisiasa na kuhakikisha waliokamatwa wanapata misaada ya kisheria na matibabu”, imeeleta taarifa hiyo.

Tamko hilo, ambalo pia linarejea matamko ya awali ya Umoja wa Ulaya (Novemba 2, 2025) na mawaziri wa mambo ya nje wa Canada, Norway na Uingereza (Oktoba 31, 2025), linaitaka Tanzania kutekeleza ahadi zake za kimataifa kuhusu uhuru wa kujieleza, haki ya kupata taarifa, na kinga za kikatiba kwa wananchi wake. Nchi hizo zimesisitiza pia umuhimu wa kutekelezwa kwa mapendekezo ya waangalizi wa uchaguzi wa AU na SADC ambao walibainisha mapungufu katika mchakato wa uchaguzi.

“Tunatambua azma ya serikali ya kudumisha amani na utulivu wa nchi, na tunasisitiza umuhimu wa vyombo vya ulinzi kutekeleza majukumu yao kwa uangalifu mkubwa. Tunarudia wito wetu kwa serikali kutekeleza ahadi zake za kimataifa za kulinda haki za msingi, ikiwemo, haki za kikatiba za kupata taarifa na uhuru wa kujieleza kwa Watanzania wote”, imeelezwa katika tamko hilo.

Tamko hilo linakuja siku chache tangu Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan alipotoa hotuba nzito jijini Dar es Salaam kueleza wazi msimamo mkali dhidi ya mashinikizo kutoka mataifa ya Magharibi. Akizungumza mbele ya wazee wa jiji hilo, Rais alisema Tanzania haitakubali kuwekewa masharti na nchi za kigeni kuhusu namna ya kuendesha masuala yake ya ndani.

“Nje huko wanakaa ooh Tanzania ifanye hivi, ifanye vile… wao kina nani? Who are you? Wanadhani wao bado ni masters wetu?” alihoji kwa ukali, akisema mashinikizo mengine hayana uhusiano na masuala ya haki bali yanachochewa na tamaa ya kutaka kufaidika na rasilimali adimu za Tanzania, ikiwemo madini na utajiri wa kiasili.

Rais Samia alionya kuwa rasilimali hizo hizo zinaweza kuwa chanzo cha migogoro ya kisiasa endapo Watanzania hawatakuwa waangalifu na wakaruhusu “macho ya nje” kuchochea mgawanyiko wa kitaifa. Alisisitiza kuwa utulivu wa nchi hauwezi kudumu endapo raia wataruhusu ushawishi wa nje kuingilia masuala yao ya ndani, akitoa wito wa mshikamano na kuepuka kuchochewa kisiasa.

Kauli za Rais zimeibua mjadala mpana ndani na nje ya nchi, zikija wakati Tanzania inapitia mijadala mikubwa kuhusu demokrasia, mageuzi ya kisiasa na nafasi ya vyombo vya dola, kufuatia kile kilichoelezwa na serikali kama “vurugu zilizopangwa” wakati wa uchaguzi na baada ya uchaguzi wa 2025.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!