Latest Posts

AIRTEL AFRIKA NA SPACEX WAINGIA UBIA WA KIMKAKATI KUUNGANISHA SATELAITI KWA SIMU

Airtel Africa imetangaza rasmi kuingia katika ushirikiano wa kimkakati na kampuni ya SpaceX ili kuanzisha huduma ya mawasiliano ya satelaiti moja kwa moja kwenye simu janja, inayojulikana kama Starlink Direct to Cell, katika nchi 14 barani Afrika ambako Airtel inahudumia zaidi ya wateja milioni 174.

Kupitia ushirikiano huu wa kihistoria, wateja wa Airtel Africa wenye simu janja zinazokidhi mahitaji ya kiteknolojia wataweza kupata huduma za mawasiliano hata wakiwa katika maeneo yasiyofikiwa na miundombinu ya kawaida ya mtandao wa ardhini. Hii ni mara ya kwanza barani Afrika huduma ya mawasiliano kutoka setilaiti hadi kwenye simu ya mkononi itapatikana kwa kiwango kikubwa, hatua inayotarajiwa kubadilisha maisha ya mamilioni ya Waafrika, hususan walioko maeneo ya mbali na magumu kufikika.

Huduma ya Starlink Direct to Cell itawezesha simu za mkononi kuunganishwa moja kwa moja na setilaiti za Starlink, mtandao mkubwa zaidi wa mawasiliano ya 4G duniani kwa upana wa kufunika maeneo mengi zaidi. Lengo kuu ni kuwafikia wananchi wanaoishi katika maeneo ambako ujenzi wa miundombinu ya mawasiliano ya ardhini umekuwa changamoto kwa muda mrefu.

Utoaji wa huduma unatarajiwa kuanza mwaka 2026, ukijumuisha huduma za ujumbe mfupi wa maandishi (SMS) na matumizi ya data kwa huduma mahsusi. Ushirikiano huu pia unajumuisha utekelezaji wa teknolojia ya kwanza ya intaneti ya kasi ya Starlink Direct to Cell, inayotumia setilaiti za kisasa zitakazowezesha simu za mkononi kupata intaneti ya kasi ya juu mara 20 zaidi ya viwango vya sasa. Utekelezaji wa huduma hii utafanyika kwa kuzingatia kikamilifu taratibu na vibali vya mamlaka za udhibiti katika kila nchi husika.

Kwa hatua hii, Airtel Africa inakuwa kampuni ya kwanza ya mawasiliano ya simu barani Afrika kuanzisha huduma ya satelaiti moja kwa moja kwenye simu janja kupitia Starlink Direct to Cell, inayotegemea zaidi ya setilaiti 650 kuwezesha mawasiliano ya kuaminika kwa wateja waliopo katika maeneo ya mbali. Ushirikiano huu unaakisi dhamira ya Airtel Africa ya kupunguza pengo la kidijitali na kuhakikisha huduma za mawasiliano zinawafikia wananchi wote bila kujali wanakoishi.

Akizungumza kuhusu ushirikiano huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Airtel Africa, Bw. Sunil Taldar, alisema:

“Airtel Africa inaendelea kujikita katika kutoa huduma bora kwa wateja wake kwa kupanua upatikanaji wa mawasiliano thabiti na yasiyokatika. Teknolojia ya Starlink Direct to Cell inaongeza nguvu kwenye miundombinu yetu ya ardhini kwa kufikia hata maeneo ambayo ni vigumu kuyahudumia kwa njia za kawaida. Tunajivunia ushirikiano huu ambao utaweka viwango vipya vya upatikanaji wa huduma katika masoko yetu yote 14.”

Kwa upande wake, Makamu wa Rais wa Mauzo wa Starlink, Bi. Stephanie Bednarek, alisema, “Kwa mara ya kwanza, watu wengi barani Afrika wataendelea kuwasiliana hata wakiwa katika maeneo ambayo mitandao ya ardhini haiwezi kufika. Tunajivunia kuona teknolojia ya Starlink Direct to Cell ikileta mabadiliko chanya katika maisha ya watu. Kupitia ushirikiano wetu na Airtel Africa, tutatoa pia teknolojia ya kizazi kipya itakayowezesha intaneti ya kasi ya juu na kurahisisha upatikanaji wa huduma muhimu.”

Ushirikiano huu unaashiria hatua kubwa katika safari ya ujumuishaji wa kidijitali barani Afrika, huku Airtel Africa na SpaceX zikiahidi kuendelea kushirikiana kubuni na kutekeleza fursa mpya zitakazochochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa wananchi wa Afrika.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!