Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza limewataka wananchi kuachana na imani potofu ikiwemo kuamini katika ushirikina ambao unaweza kuchochea mauaji, ukatili na matukio mengine ya jinai katika baadhi ya maeneo, hususan katika Kisiwa cha Ukara, Wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza.
Kauli hiyo imetolewa Disemba 17, 2025 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, DCP Wilbrod Mutafungwa, alipofanya mkutano wa hadhara na wakazi wa Kata ya Bwisya wilayani humo kwa lengo la kutoa elimu ya usalama na kuhimiza utunzaji wa amani.
Akizungumza kwenye mkutano huo uliowakutanisha viongozi wa Serikali, dini na wananchi, DCP Mutafungwa amesema jukumu la kudumisha amani ni la kila mmoja, hivyo kila mmoja anapaswa kushiriki kikamilifu kukemea vitendo vya uvunjifu wa amani vinavyofanywa na watu wanaojiita wataalam wa kusaka wachawi maarufu kama ‘Kamchape’.

Amebainisha kuwa kundi hilo limekuwa likijihusisha na uporaji wa mali, utapeli kwa kutumia ramli chonganishi na kuingia katika nyumba za watu kwa madai ya kuondoa ushirikina jambo ambalo linajenga chuki na kukiuka sheria za nchi.
“Hatutaruhusu watu binafsi au viongozi kuwatapeli wananchi kwa kisingizio cha matambiko au imani za kishirikina. Jeshi la Polisi liko tayari kulinda raia na mali zao wakati wote,” amesema Kamanda Mutafungwa.

Ametoa wito kwa wananchi kuacha kuwahifadhi wahalifu hao (Kamchape)badala yake watoe ushirikiano kwa Jeshi la Polisi ili hatua kali zichukuliwe dhidi yao kwa mujibu wa sheria.
Aidha, Kamanda Mutafungwa amesema watu 21 wanashikiliwa na Jeshi la Polisi wakihusishwa na vitendo hivyo vya kihalifu na uchunguzi dhidi yao unaendelea, utakapokamilika watafikishwa kwenye vyombo vya sheria.
Kwa upande wao, baadhi ya wananchi wa Kisiwa cha Ukara, akiwemo Maritha Nyangeta na Samsoni Ibrahim, wamelishukuru Jeshi la Polisi kwa kufika kisiwani hapo na kutoa elimu, wakisema hatua hiyo imewaondolea hofu waliyoishi nayo kwa zaidi ya miezi mitatu.

Wamesema wamekuwa wakilengwa na kundi la Kamchape linalopita nyumba kwa nyumba, kuwatisha na kuwanyang’anya mali zao kwa madai ya kuwatoa uchawi, hali iliyozua taharuki na kuathiri maisha yao ya kila siku.
Jeshi la Polisi limeahidi kuendelea na msako mkali dhidi ya watu wote wanaojihusisha na vitendo hivyo hadi pale vitakapotokomezwa.
Mkutano huu umejiri ikiwa ni siku chache baada ya maandamano kujitokeza katika Kisiwa cha Ukara wilayani Ukerewe mkoani Mwanza kutokana na mvutano kati ya wananchi na baadhi ya viongozi wa vijiji na vitongoji kuhusu ujio wa kundi linalojulikana kama Kamchape, linalodaiwa kujihusisha na kuondoa vitendo vya uchawi na ushirikina.
Kamchape ni kikundi cha watu ambacho kimekuwa kikidaiwa kuwa na uwezo na lengo la kupambana na vitendo vya uchawi na imani za kishirikina ikiwemo maarufu kama “chuma ulete”, jambo ambalo limepata uungwaji mkono mkubwa kutoka kwa wananchi wa Ukara, huku kikipingwa na baadhi ya viongozi wa ngazi ya chini katika kisiwa hicho.
Tarehe 14 Desemba 2025, wakazi wa Kitongoji cha Kwilela, Kata ya Bwisya, waliandamana hadi Kituo cha Polisi Bwisya baada ya kuitwa kufuatia malalamiko yaliyotolewa na Mwenyekiti wa Kitongoji hicho, akiwashitaki kwa kufanya kikao cha kuchangisha fedha kwa ajili ya kumleta Kamchape bila idhini yake. Baada ya kufika kituoni, pande zote zilipatanishwa na kukubaliana kuruhusu Kamchape kufanya shughuli zake, ingawa hadi sasa zoezi hilo bado halijatekelezwa katika kitongoji hicho.
Hata hivyo, hali ilizidi kuwa tete leo tarehe 15 Desemba 2025 katika Kitongoji cha Ebhugwe, Kata ya Bwisya, ambapo shughuli ya Kamchape ilikuwa ikiendelea kabla ya kuzuiwa na kundi la watu saba likiongozwa na Mwenyekiti Mstaafu wa Kitongoji cha Ebhugwe, Ndg. Paschal, pamoja na Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kwilela. Hatua hiyo ilisababisha mvutano mkali kati yao na wananchi waliokuwa wakishuhudia zoezi hilo.
Wananchi walifanikiwa kulitawanya kundi hilo, lakini kutokana na hali ya taharuki, zoezi la kuondoa ushirikina lilisitishwa kwa siku ya leo, huku maandamano yakiripotiwa kuendelea katika maeneo mbalimbali ya kisiwa hicho wakidai kuruhusiwa kwa shughuli za Kamchape.
Waandamanaji walisema baada ya zoezi la kuondoa ushirikina kukamilika, wanapanga kufanya maandamano makubwa zaidi wakidai kujiuzulu kwa wenyeviti wa vitongoji na vijiji wanaopinga Kamchape, wakisisitiza kuwa kwao Kamchape ni hatua ya “ukombozi wa jamii” dhidi ya ushirikina unaodaiwa kuathiri maisha na ustawi wao.