Latest Posts

WENYE ULEMAVU WANUFAIKA MGODI WA MSASA

Mikakati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inalenga kuhakikisha makundi maalum yakiwemo vijana, wanawake na watu wenye ulemavu yanashiriki na kunufaika na rasilimali zilizopo nchini.

Katika kutekeleza azma hiyo, Mgodi wa Wachimbaji Wadogo wa Msasa uliopo wilayani Bukombe umeendelea kuwa mfano kwa kutoa fursa kwa watu wenye ulemavu kushiriki shughuli za uchimbaji, pamoja na kuwaondolea baadhi ya kodi na tozo zisizo za lazima.

Mgodi huo ulianza shughuli za uchimbaji tarehe 21 Oktoba 2025, awali ukiwa katika mfumo wa rush, kabla ya kupatiwa leseni rasmi. Kwa sasa, mgodi huo umeanza uzalishaji na unakadiriwa kutoa ajira kwa watu kati ya elfu sita hadi elfu nane wanaojishughulisha katika shughuli mbalimbali za uchimbaji.

Tofauti na migodi mingine, uongozi wa Mgodi wa Msasa umehakikisha kundi la watu wenye mahitaji maalum halisahauliki kwa kuwapatia shughuli zinazolingana na uwezo wao, jambo linalothibitishwa na baadhi ya walengwa hao.

Miongoni mwa wanufaika hao ni Mageta Matinde, mchimbaji mdogo mwenye ulemavu uliotokana na ajali ya kuangukiwa na duara mwaka 1998. Mageta anasema licha ya kuzunguka migodi mbalimbali, Mgodi wa Msasa umeonesha utofauti mkubwa kwa namna unavyowajali na kuwajumuisha watu wenye ulemavu katika shughuli za uchimbaji.

Hata hivyo, pamoja na mafanikio hayo, eneo la Mgodi wa Wachimbaji Wadogo Msasa bado linakabiliwa na changamoto ya usalama barabarani, kutokana na mgodi huo kuwa pembezoni mwa barabara kuu inayounganisha Tanzania na mataifa jirani.

Akizungumza kuhusu changamoto hiyo, Meneja wa mgodi huo, Laurent Mgasha, ameziomba mamlaka husika kuchukua hatua za haraka za kuimarisha usalama barabarani ili kuzuia ajali za mara kwa mara zinazohatarisha maisha ya wachimbaji na wananchi wanaopita katika eneo hilo.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!