Latest Posts

NHC YAKABIDHI ZAWADI KWA WAHITIMU CHUO CHA ARDHI

Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limeendelea kudhihirisha dhamira yake ya dhati katika kukuza ubora wa elimu ya juu na kuibua vipaji vya kitaaluma baada ya kuwakabidhi zawadi wanafunzi bora wa Chuo Kikuu cha Ardhi (ARU) jijini Dar es Salaam, waliobobea katika masomo mbalimbali ya miliki kuu kwa mwaka wa masomo 2024/2025.

Hafla hiyo ya kukabidhi zawadi ilifanyika Disemba 16, 2025, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa muda mrefu wa NHC Academic Prizes unaolenga kuwatambua, kuwahamasisha na kuthamini wanafunzi wanaofanya vizuri zaidi kitaaluma katika fani zinazohusiana moja kwa moja na sekta ya ardhi, mali isiyohamishika na usimamizi wa majengo.

Kupitia mpango huo ulioanza mwaka 2014, wanafunzi kutoka programu mbalimbali wamekuwa wakipokea zawadi za fedha kama ishara ya kutambua juhudi, nidhamu na ubora wao wa kitaaluma. Kwa mwaka huu, wanafunzi wa kuanzia mwaka wa kwanza hadi wa mwisho katika programu za BSc. Property and Facilities Management (PFM), BSc. Real Estate Finance and Investment (REFI) pamoja na BSc. Land Management and Valuation (LMV) wamenufaika na tuzo hizo.

Vigezo vya ushindi vilijikita katika utendaji wa jumla wa kitaaluma, ubora katika masomo maalum pamoja na uwezo wa kitaalamu unaoandaliwa kwa ajili ya soko la ajira. Katika hatua hiyo, wanafunzi waliobobea katika masomo ya msingi yakiwemo Housing, Valuation Casework, Corporate Real Estate Management, Real Estate Market Analysis, Facilities Management pamoja na Professional Casework walipata tuzo zenye thamani tofauti kulingana na ngazi na mchango wa masomo husika katika maandalizi ya taaluma zao za baadaye.

Zawadi za NHC zenye jumla ya thamani ya shilingi milioni nne zilitolewa na Meneja wa Habari na Uhusiano wa Shirika hilo, Muungano Saguya, kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa NHC. Akizungumza baada ya kukabidhi tuzo hizo, Saguya alisema NHC imekuwa ikitoa zawadi hizo kila mwaka kama njia ya kuchochea ufaulu, kuongeza morali ya kujifunza na kuandaa rasilimali watu mahiri kwa ajili ya sekta ya makazi na mali isiyohamishika.

Kwa upande wake, Jephta Clemence, mmoja wa wanafunzi bora na mhitimu wa Shahada ya Sayansi ya Mifumo ya Taarifa za Kijiografia na Uchanganuzi wa Anga (GIS and Remote Sensing), alisema kupokea tuzo hiyo ni faraja kubwa kwake na motisha kwa wanafunzi wengine.

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Ardhi, Profesa Evaristo Liwa, amepongeza hatua ya NHC kuendelea kutoa tuzo hizo, akisema ni mchango mkubwa katika kuongeza hamasa ya wanafunzi kitaaluma. Ameeleza kuwa kwa mwaka huu, NHC imeongeza idadi ya tuzo kutoka moja hadi kufikia tisa, hatua aliyosema inaonesha dhamira ya kweli ya kuwekeza katika elimu.

“kuna wengine walikuwa wanatoa zawadi kwa mapenzi yao binafsi, mfano NHC wana zawadi karibu 9 lakini zamani walikuwa wana zawadi moja”, alisema Prof. Liwa.

Kwa kutoa tuzo hizo, NHC inalenga si tu kuhamasisha ushindani chanya wa kitaaluma, bali pia kuhakikisha inachangia kikamilifu katika maandalizi ya rasilimali watu wenye ujuzi, weledi na ubunifu watakaokuja kuimarisha sekta ya makazi, mali isiyohamishika na maendeleo ya miji nchini.

Mpango huo unaakisi dira ya NHC ya kuwekeza katika maarifa kama nguzo muhimu ya maendeleo endelevu ya Taifa, na kuthibitisha kuwa shirika hilo halijikita tu katika ujenzi wa nyumba na miundombinu ya kisasa, bali pia katika kujenga misingi imara ya utaalamu na maarifa kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Aidha, imeelezwa kuwa wanafunzi wengi wa Chuo Kikuu cha Ardhi hupata fursa ya kufanya mafunzo kwa vitendo katika Shirika la Nyumba la Taifa, jambo linaloifanya NHC kuwa daraja muhimu la kutoa ujuzi, uzoefu na maandalizi ya kitaaluma kwa wanafunzi na wahitimu, ambao baadaye huwa hazina muhimu katika tasnia ya majengo na maendeleo ya Taifa kwa ujumla.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!