Latest Posts

MRADI WA TACTIC KUONGEZA MTANDAO WA BARABARA ZA LAMI MTWARA

Mradi wa Uboreshaji wa Miundombinu ya Miji ya Tanzania (TACTIC) umeendelea kuwa chachu ya maendeleo kwa wananchi wa Manispaa ya Mtwara Mikindani, kwa kutoa fursa za ajira na kuboresha miundombinu ya barabara na mifereji ya maji, hatua inayochochea ustawi wa kiuchumi na kijamii katika eneo hilo.

Kupitia mradi huo unaoratibiwa na Mamlaka ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), barabara kadhaa za kiwango cha lami zinajengwa na kukarabatiwa, hali inayochangia kurahisisha usafiri, kuongeza thamani ya maeneo husika na kuboresha mazingira ya biashara kwa wakazi wa manispaa hiyo.

Akizungumza wakati wa utekelezaji wa mradi, Meneja wa TARURA Wilaya ya Mtwara Mhandisi Hatibu Nunu, amesema kuwa mradi wa TACTIC unalenga sio tu kuboresha barabara bali pia kupanua mtandao wa barabara za lami ndani ya Manispaa ya Mtwara Mikindani, ambapo kilomita 6 zinaongezwa na kufikisha jumla ya kilomita 60 za barabara za lami.

Mbali na ujenzi wa barabara, mradi huo umezingatia pia ajira kwa wananchi wa maeneo husika. Mhandisi Mshauri Mkazi wa miradi ya TACTIC, Henry Moshi amesema kuwa utekelezaji wa mradi umeambatana na uanzishwaji wa maabara ya kupima ubora wa vifaa vya ujenzi, jambo litakalosaidia miradi mingine ya ujenzi ndani na nje ya manispaa.

Ameeleza kuwa mkazo umewekwa katika kuajiri vibarua kutoka jamii zinazozunguka miradi hiyo ili kuhakikisha wananchi wananufaika moja kwa moja.

Wananchi nao wameonesha kuridhishwa na mradi huo miongoni mwao ni Yohana Peter, ambaye ni mmoja wa wanufaika, amesema kuwa mradi wa TACTIC umechangia kuwaongezea kipato wananchi na kupunguza ukosefu wa ajira, hasa kwa vijana na ameeleza kuwa ujio wa mradi huo umeleta matumaini mapya na kuhimiza vijana kutumia fursa zilizopo kujijenga kiuchumi.

Kwa ujumla, mradi wa TACTIC umeendelea kudhihirisha dhamira ya serikali katika kuboresha miundombinu ya miji na kuinua maisha ya wananchi kupitia miradi yenye tija, hususan katika Manispaa ya Mtwara Mikindani.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!