Latest Posts

POLISI YAWAHIMIZA WANANCHI KUZINGATIA USHIRIKIANO NA TAHADHARI KIPINDI CHA SIKUKUU MTWARA

Jeshi la Polisi mkoani Mtwara limewahimiza wananchi kuendelea kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kwa kuzingatia sheria na kutoa taarifa za kiusalama, ili kudumisha amani na utulivu wakati wa sikukuu za Krismas na Mwaka Mpya.

Wito huo umetolewa leo Disemba 24,2025 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, SACP Issa Sulemani wakati akizungumza na waandishi wa habari mkoani humo, ambapo amesema jeshi hilo limejipanga kikamilifu kuhakikisha usalama wa wananchi unaendelea kuwa wa uhakika katika kipindi chote cha sikukuu za mwisho wa mwaka.

Amesema Polisi kwa kushirikiana na wananchi pamoja na vyombo vingine vya dola wanaendelea kufanya doria katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo, ikiwemo maeneo ya fukwe, mitaa ya katikati ya miji pamoja na maeneo ya pembezoni ili kuzuia na kudhibiti vitendo vyovyote vinavyoweza kuhatarisha usalama.

Kamanda Sulemani amesema kwa sasa hali ya usalama mkoani Mtwara ni shwari, huku akisisitiza kuwa jeshi hilo liko tayari kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya mtu yeyote atakayejihusisha na vitendo vya uvunjifu wa amani, uhalifu wa kijamii au ukiukwaji wa sheria za usalama barabarani.

Aidha, amewatahadharisha madereva wanaopuuzia sheria za usalama barabarani kuwa hawatasita kuchukuliwa hatua za haraka, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuzuia ajali kipindi cha sikukuu.

Pia Jeshi la Polisi limewataka wazazi na walezi kuongeza uangalizi kwa watoto wao, kwa kuepuka kuwaacha kwenda kwenye kumbi na maeneo ya starehe bila uangalizi, ili kuwalinda dhidi ya hatari za kupotea, ajali pamoja na vitendo vya ukatili na udhalilishaji vinavyoweza kuhatarisha afya na maisha yao.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!