Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba, Jamal Dadi, amekabidhi msaada wa vyakula na mahitaji mbalimbali vyenye thamani ya Shilingi milioni 2 kwa kituo cha kulelea watoto yatima cha Mbingu Sisters,ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, la kuwajali watoto wenye mahitaji maalum ndani ya siku 100 za uongozi wake.
Akizungumza Desemba 24, 2025, wakati wa hafla ya makabidhiano iliyofanyika katika kituo hicho, Dadi amesema Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuonyesha dhamira ya dhati ya kuwajali watoto yatima na wale walio katika mazingira magumu, kwa kuhakikisha wanapata huduma za msingi za maisha na malezi bora.

Aidha, ameitaka jamii kutambua kuwa watoto hao ni sehemu ya rasilimali ya taifa, na kuwalea vyema ni kuandaa kizazi cha viongozi na raia wema wa baadaye.
Kwa upande wake, Sista mlezi wa kituo hicho, Maria Sapiencia, ameishukuru Serikali kupitia Halmashauri ya Mlimba kwa moyo wa upendo waliouonyesha kwa watoto hao, akieleza kuwa msaada huo utasaidia kwa kiasi kikubwa katika kuimarisha huduma za malezi na ustawi wa watoto wanaolelewa hapo.