Jamii imeaswa kutenda matendo mema, hususan kuwahudumia watu wenye uhitaji wakiwemo yatima, wajane na watu wasio na uwezo, katika msimu huu wa sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya.
Wito huo umetolewa na Sospete Kinasa kutoka Shirika la Bima la Milembe Insurance, tawi la Geita Mjini, wakati wakitoa zawadi za Krismasi kwa kituo cha watoto yatima cha Moyo wa Huruma kilichopo mjini Geita.

Amesema ni muhimu kwa watoto waliopo katika kituo hicho kuzingatia elimu pamoja na kushiriki kikamilifu katika kumjua Mungu zaidi, kwani misingi hiyo itawasaidia kujijenga kwa maisha ya baadaye.
Aidha, amewahimiza Watanzania kujenga utamaduni wa kusherehekea sikukuu kwa kuwajumuisha watoto wasio na uwezo, kwa kuwapenda, kushirikiana nao na kuwatembelea mara kwa mara.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa kituo hicho, Sista Maria Lahuda, amesema kituo cha Moyo wa Huruma ni makao salama kwa watoto yatima na kwamba wameendelea kuwalea kwa misingi ya kumpendeza Mungu. Ameongeza kuwa kituo hicho kimefanikiwa kuwawezesha baadhi ya watoto kufikia ngazi ya elimu ya juu ikiwemo vyuo vikuu na wengine kuendelea na masomo ya shule za msingi.

Sanjari na hilo, Milembe Insurance imetoa zawadi pamoja na hati za pongezi kwa wateja wake waliofanya vizuri katika mwaka huu, ikiwa ni sehemu ya kutambua na kuthamini ushirikiano wao.