Mbunge wa Jimbo la Mtwara Vijijini Arif Suleiman Premji, amekiomba Chama Kikuu cha Ushirika kinachohudumia wilaya za Nanyumbu, Masasi na Mtwara (MAMCU) kuunda dawati maalumu litakaloshughulikia changamoto mbalimbali za wakulima, ikiwemo suala la bei ndogo ya mazao katika jimbo hilo.

Akizungumza leo Desemba 29, 2025, katika mnada wa nane na wa mwisho wa zao la korosho unaoendeshwa kupitia Chama cha MAMCU, Arif amesema kuwa ukiangalia takwimu za bei na kuzilinganisha na majimbo mengine, bei ya korosho katika Jimbo la Mtwara Vijijini iko chini, hali iliyomlazimu kuomba kuundwa kwa dawati hilo maalumu ili kujadili na kutafuta namna ya kutatua changamoto hiyo.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Abdallah Mwaipaya ameunga mkono hoja ya Mbunge wa Jimbo la Mtwara Vijijini, Arif Suleiman Premji, ya kuundwa kwa dawati hilo kwa lengo la kufanya tathmini ya changamoto mbalimbali zilizojitokeza kwa wakulima.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika cha MAMCU, Alhaji Azam Mfaume, amesema kuwa ili wakulima waweze kunufaika kikamilifu, ni lazima zao la korosho lifanywe kuwa biashara na kuacha kulichanganya na mambo mengine na kuongeza kuwa chama hicho kimekubaliana na kauli ya Mbunge Arif ya kuundwa kwa dawati maalumu litakaloshughulikia masuala ya korosho mkoani Mtwara.

Kwa upande wake, Meneja wa Chama hicho Biadia Matipa, amesema hadi sasa wakulima wote wameshalipwa fedha zao, ambapo zaidi ya shilingi bilioni 274 zimewafikia wakulima. Aidha, amewaomba wakulima wenye changamoto za malipo kufika katika ofisi za chama hicho ili changamoto zao zipatiwe ufumbuzi.

Katika mnada huo Mamcu wamefanikiwa kuuza korosho zaidi ya tani elfu 80 ambapo bei ya juu ni shilingi elfu 2,280 na bei ya chini ni shilingi elfu 1,810 na kupelekea kuuza korosho tani 112,000 kwa msimu wa 2025,2026.