Latest Posts

MHANDISI KUNDO AMPA SIKU 60 MKANDARASI KUKAMILISHA KAZI SERENGETI

Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Kundo Mathew, ameagiza kilometa 30 za mtandao wa mabomba katika Mradi wa Maji wa Miji 28 wilayani Serengeti zikamilishwe ndani ya siku 60, kufuatia kutoridhishwa na kasi ya utekelezaji wa mradi huo.

Akizungumza wakati wa ziara ya kukagua mradi huo, Mhandisi Kundo amesema mradi huo ulipaswa kukamilika Aprili 2025, hivyo ucheleweshaji uliopo haukubaliki. Amesisitiza kuwa serikali imetekeleza wajibu wake kikamilifu kwa kutoa fedha kwa wakati, jambo lililotarajiwa kusaidia mradi kukamilika kwa mujibu wa mpango.

Mhandisi Kundo amebainisha kuwa changamoto zinazosababisha kuchelewa kwa mradi zinatokana na mkandarasi, zikiwemo kuwa na idadi ndogo ya wafanyakazi wasiokidhi mahitaji ya mkataba, baadhi yao kukosa sifa stahiki, kuchelewa kununua vifaa pamoja na kushindwa kuwalipa wafanyakazi kwa wakati.

Kutokana na hali hiyo, amemuagiza mkandarasi kampuni ya Mega Engineering and Infrastructure Company Ltd kuongeza idadi ya wafanyakazi mara moja na kuwasilisha orodha ya wafanyakazi wote pamoja na taarifa za malipo yao ya kila mwezi katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ili kuondoa malalamiko yanayoendelea kutoka kwa wafanyakazi.

Aidha, Mhandisi Kundo amesisitiza kuwa ndani ya siku 14, vifaa vyote vinavyohitajika kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo viwe vimewasili eneo la kazi. Mradi wa Maji wa Miji 28 wilayani Serengeti unatekelezwa kwa gharama ya shilingi bilioni 21 na unatarajiwa kuwahudumia wananchi takribani 166,000 mara utakapokamilika.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!