Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima, amewataka wataalam wanaojishughulisha na upimaji wa afya ya udongo kutumia tafiti zao za kisayansi kuongeza tija katika kilimo na kuchochea maendeleo ya kiuchumi wa Mkoa huo na taifa kwa ujumla.
Malima ametoa kauli hiyo Januari 8, 2026 alipokutana na wataalam wa afya ya udongo ofisini kwake na kujadili masuala mbalimbali yanayohusu namna ya kuendelea kuifanya Morogoro kuwa mkoa wa kimkakati hususan katika sekta ya kilimo.

Mkuu huyo wa Mkoa amesisitiza kuwa matumizi ya maarifa ya kitaalamu ndiyo njia sahihi ya kuongeza uzalishaji wa mazao, kupunguza gharama kwa wakulima na kuhakikisha matumizi bora ya pembejeo yanazingatiwa na wakulima.
Aidha amesema, tafiti za afya ya udongo zitaenda kuchagiza utekelezaji wa mkakati wa mkoa wa Morogoro wa kuhakikisha mazao ya kimkakati yakiwemo kakao, karafuu, parachichi, mchikichi na mazao mengine yanastawi Mkoani humo kwa lengo la kuwanufaisha wananchi hivyo, akataka ushirikiano wao na kuahidi kuwapa usaidizi watakaouhitaji.
“… Mimi nawaombeni mtakapoenda kufanya tafiti huko, mkikutana na jambo lolote zito mniambie…” — amesisitiza Malima.
Katika hatua nyingine kiongozi huyo ameomba Mkoa huo kupewa kipaumbele katika zoezi hilo la kitaifa la upimaji wa afya ya udongo kutokana na mkoa huo kuwa kitovu cha uzalishaji wa mazao ya kimkakati yaliyobainishwa hapo juu ambayo yanachangia kwa kiasi kikubwa uchumi wa Taifa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Usimamizi wa Matumizi ya Ardhi kutoka Wizara ya Kilimo, Mhandisi Florian Kalemera amesema zoezi hilo tayari limekamilika katika mikoa 13 ya Tanzania Bara na kwa sasa linaendelea katika mikoa sita ya Morogoro, Pwani, Tanga, Tabora, Lindi na Mtwara.

Amesema lengo kuu la zoezi hilo ni kuhakikisha kila mkulima anapata taarifa sahihi kuhusu hali ya udongo wake ili kufanya maamuzi sahihi ya kilimo kwa kuzingatia aina ya mazao na virutubisho vinavyohitajika kulingana na mahitaji halisi ya udongo husika.