Latest Posts

TANZANIA YAJIVUNIA KUWA NCHI INAYOENDELEA KUKOPESHEKA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameelezea kufurahishwa kwake na hatua ya mashirika makubwa ya kimataifa ya Moody’s na Fitch kuendelea kuipa Tanzania alama za daraja la juu la mkopo (B1 na B+), jambo ambalo limesaidia kujenga imani kubwa kwa wawekezaji na kushusha gharama za ukopaji kwa taifa. Mashirika hayo yanajihusisha na kutathimini uwezo wa nchi kuyafikia masoko ya fedha ya kimataifa na kukopesheka katika masoko ya mitaji ya kimataifa.

Akihutubia mabalozi na wakuu wa mashirika ya kimataifa leo, Januari 15, 2026, katika hafla ya Diplomatic Sherry Party Ikulu Chamwino, Rais Samia amesema alama hizo nzuri zimekuwa kichocheo kikubwa cha mafanikio ya kiuchumi yaliyoshuhudiwa mwishoni mwa mwaka 2025.

“Tumeendelea kufurahia daraja nzuri la mikopo la B1 kutoka Moody na B+ kutoka Fitch. Mtazamo huu thabiti unaashiria imani ya wawekezaji, gharama nafuu za mikopo, na ustahimilivu wa kiuchumi, jambo ambalo ni hatua chanya katika kujenga imani ya kimataifa na kuvutia uwekezaji zaidi wa kigeni (FDI). Tunajitahidi kuhakikisha mageuzi endelevu ya kiutawala, kupunguza uhaba wa fedha za kigeni, na kuboresha uwiano wa kodi kwa Pato la Taifa (GDP)”, amesema Rais Samia.

Alama hizo nzuri zimeelezwa kutafsiriwa kwa vitendo ambapo hadi kufikia Desemba 2025, Tanzania imevunja rekodi ya kihistoria kwa kusajili miradi mipya ya uwekezaji 927 yenye thamani ya zaidi ya Dola za Kimarekani bilioni 11.09. Hii ni ongezeko la asilimia 19.03 kulinganisha na mwaka uliotangulia.

“Mwaka 2025, Tanzania ilisajili miradi mipya ya uwekezaji 927 yenye thamani ya zaidi ya Dola za Marekani bilioni 11, miradi inayotarajiwa kutoa ajira zaidi ya 162,000 kwa Watanzania.” amesema Rais Samia na kuongeza,

“Wakati uwekezaji wa kigeni (FDI) ukiendelea kuwa imara, ushiriki wa wawekezaji wa ndani pia umeendelea kuwa na nguvu, kukiwa na miradi 288 (sawa na asilimia 31.07) inayotarajiwa kutekelezwa na wawekezaji wa ndani. Hii inaonesha kukua kwa imani miongoni mwa wajasiriamali wa Kitanzania. Kwa wawekezaji wetu, tunaahidi kuhakikisha kuwa uwekezaji uliopo na ule mpya unalindwa na kuimarishwa”.

Rais Samia amewahakikishia wawekezaji kuwa serikali italinda uwekezaji wao na inaendelea kufanya mageuzi ya kiutawala ili kutatua changamoto ya uhaba wa fedha za kigeni. Aidha, amesisitiza kuwa Tanzania itaendelea kuimarisha amani na mshikamano ndani ya EAC, SADC na AU, kwani maendeleo hayawezekani bila utulivu wa kikanda.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!