Hali ya sintofahamu imeanza kutanda katika sekta ya usafirishaji jijini Dar es Salaam, hususan katika Barabara ya Kilwa, kufuatia ombi la Kampuni ya Mofat inayotoa huduma ya mabasi yaendayo haraka kuitaka Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) kuziondoa daladala, bajaji, na bodaboda katika njia hiyo ili ibaki pekee kutoa huduma za usafiri kwa njia hiyo.
Tovuti ya Mwananchi imeripoti kuwa tangu kuanza kwa huduma hiyo Oktoba 2025, Mofat inadai kupata hasara kubwa, hali iliyopelekea kuegesha mabasi 160 kati ya 200 yaliyopo, huku mabasi 40 pekee yakiwa barabarani. Ofisa Mkuu wa Uendeshaji wa Mofat, Mabrouk Masasi, ameeleza kuwa ushindani kutoka kwa daladala umesababisha wakose abiria wa kutosha kurejesha mikopo na kulipa mishahara ya madereva 187.
“Kutokana na kufanya kazi sambamba na vyombo hivyo vya, tumejikuta tukigawana abiria waliopo na hivyo hakuna faida tunayoipata na pia ndio maana tumeshindwa kuongeza magari mengine barabarani kwani mpaka sasa ni 40 tu ndio yaliyo barabarani huku 160 yakiwa yameekeshwa”, amenukuliwa Mabrouk katika taarifa hiyo.

Hata hivyo, ombi hilo limepokewa kwa upinzani mkali kutoka kwa wananchi na wadau wa usafiri ambao wanahofia kuwa kuiondoa daladala kutaibua adha kubwa kama ile iliyoshuhudiwa katika Barabara ya Morogoro miaka ya nyuma. Wakazi wa maeneo ya Toangoma, Chamazi, na Mbagala wamebainisha kuwa mabasi ya mwendokasi yanatoza nauli ya Shilingi 1,000, gharama ambayo ni kubwa kwa wananchi wa kipato cha chini ukilinganisha na Shilingi 500 au 700 inayotozwa na daladala.
Aidha, wadau wamehoji mantiki ya kampuni hiyo kulalamikia hasara wakati inatumia miundombinu maalum isiyo na foleni na nishati ya gesi ambayo ni nafuu, huku wakidai kuwa usafiri huo bado haujafika maeneo mengi ya mbali ambayo daladala zinahudumia moja kwa moja bila mabadilisho ya magari.
“Ifike mahali mwendokasi wasitake kujiona wao ni bora kuliko wasafirishaji wengine, maana kila upendeleo wamepewa kuanzia miundombinu,” amesema Anord Kelvin, Mkazi wa Toangoma
Kwa upande mwingine, viongozi wa vyama vya madereva na wasafirishaji wametahadharisha kuwa kuiondoa sekta ya bajaji na bodaboda kutapoteza ajira za zaidi ya vijana 200,000, jambo linaloweza kuchochea ongezeko la uhalifu mitaani. Wanashauri kuwa badala ya kutafuta ukiritimba wa kibiashara, kampuni ya Mofat inapaswa kuboresha huduma zake na kushirikiana na wasafirishaji wadogo kama “Feeder” wa abiria kutoka mitaani kuelekea vituo vikuu.
“Kibiashara kuondolewa kwa daladala ni sawa lakini kihuduma sio sawa, kwani ukisema leo daladala ziondolewe kwa haraka yatatokea kama yale ya Kimara ambapo wananchi walipaza sauti hadi kuleta vurugu walipoona changamoto wanazozipata kwenye usafiri huo wa mwendokasi hazisikilizwi”, ameeleza Katibu wa Chama cha Madereva Tanzania (TADWU), Ramadhan Seleman.
Wakati mvutano huo ukiendelea, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano kwa Umma Latra, Salum Pazzy alikiri wamepokea nakala ya barua kutoka Mofat na kueleza wapo wanaifanyia kazi kwa kuwa ni jambo linalotakiwa kuwashirikisha na wadau wengine katika sekta hiyo ya usafirishaji.