Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga, Nyakia Ally Chirukile, amewataka wafanyabiashara kufanya makadirio na malipo ya kodi kwa wakati ili kuchangia maendeleo ya taifa.
Akizungumza leo tarehe 20.01.2026 katika ofisi yake alipokutana na timu ya maafisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa lengo la kujitambulisha na kutangaza zoezi la utoaji elimu ya kodi mlango kwa mlango litakaloanza tarehe 20.01.2026 hadi tarehe 30.01.2026 katika mkoa wa Rukwa. Chirukile amesema ulipaji wa kodi umechangia sana maendeleo ya nchi.


“Niwatake wafanyabiashara wote kufanya makadirio ya kodi na malipo ya kodi kwa wakati ili tuzidi kukuza uchumi na maendeleo ya nchi” amesema Chirukile.
Pia Chirukile amewataka wafanyabiashara kutoa ushirikiano kwa timu ya elimu itakayopita maeneo yao ya biashara kwa lengo la kutoa elimu ya kodi na kuchukua mrejesho wa maoni kutoka kwa wafanyabiashara jambo ambalo litawezesha kuongeza uelewa sahihi na kuboresha mifumo ya ukusanyaji wa kodi.
Kwa upande wake, Kiongozi wa timu ya uelimishaji na Afisa Uhusiano Mkuu wa TRA, Bw. Macdonald Mwakasendile amesema zoezi la elimu ya kodi mlango kwa mlango limekuwa likifanyika kwa miaka kadhaa na limefanikiwa kuongeza ushirikiano kati ya wafanyabiashara na TRA pamoja na kuongeza uelewa kwa umma kuhusu wajibu wa kodi.

“Tunawaomba wafanyabiashara kutumia fursa hii kupata Elimu ya kodi, kupata majibu ya maswali yao, kutoa maoni na ushauri ili kuboresha huduma zetu.” amesema Bw. Mwakasendile.
TRA imekuwa ikiendesha zoezi la elimu ya kodi mlango kwa mlango kwa kuwatembelea wafanyabiashara katika maeneo yao ya biashara jambo ambalo limeongeza ushirikiano baina ya wafanyabiashara na TRA na limeongeza uelewa mpana juu ya masuala ya kodi.