Latest Posts

‘A TO Z’ KESI YA UHAINI YA LISSU, JAMHURI ‘YATAKA’ KUPELEKA MASHAHIDI WA SIRI MAHAKAMA KUU

Na; mwandishi wetu

Kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Taifa Tundu Lissu imeendelea leo, Jumanne Julai 15.2025 kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam ambapo ilikuja kwa ajili ya kutajwa

Katika kesi hiyo ambayo mtuhumiwa Tundu Lissu ambaye kiuhalisia ni mbobezi wa masuala ya sheria anajitetea mwenyewe, ilianza kwa Wakili wa Serikali Mkuu Nossor Katuga anayeongoza jopo la Mawakili wa Jamhuri,  kuieleza Mahakama kuwa shauri hilo lipo kwenye hatua ya kusomwa na kutolewa maamuzi, na kwamba kwa sasa baada ya upelelezi kukamilika, jalada la shauri husika lilipelekwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) ambaye amelipitia na kujiridhisha na ushahidi uliopo, na kwamba kwakuwa ameona ushahidi huo umejitosheleza sasa shauri hilo lipo tayari kupelekewa Mahakama Kuu kwa ajili ya kuanza kusikilizwa

Wakili Katuga, aliendelea kuieleza Mahakama kuwa kufuatia maoni hayo ya DPP, Jamhuri sasa imewasilisha maombi Mahakama Kuu ambayo yanapaswa kusikilizwa kabla ya kupelekwa kwa kesi ya msingi, ambapo amesema maombi hayo ambayo yamepokelewa na kupewa namba 17059 ya mwaka 2025, yamepelekwa kwa kutumia kifungu cha 124 cha sheria ya makosa ya jinai sura ya 20 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2023

Maombi yaliyowasilishwa na Jamhuri Mahakama Kuu ni yale ya kutaka ‘kuficha’ baadhi ya taarifa zinazopelekea kutambulika kwa mashahidi ikilenga kuwaleta ‘mashahidi (baadhi) wa siri’

Kufuatia kuwasilisha taarifa hiyo Mahakamani hapo, Wakili wa Serikali Mkuu Nassor Katuga aliiomba Mahakama kuhairisha shauri hilo hadi tarehe nyingine ili kutoa nafasi kwa Mahakama Kuu kusikiliza maombi hayo na kutolea maamuzi, ambapo katika ujenzi wa hoja yake aliieleza Mahakama kuwa Jamhuri imefikia maamuzi ya kuwasilisha maombi hayo Mahakama Kuu ili kulinda usalama wa mashahidi wake, na kwamba hairisho la shauri hilo wanaliwasilisha kwa kutumia kifungu cha 265

Hoja hiyo ilipingwa vikali na mshtakiwa Tundu Lissu ambapo aliieleza Mahakama kuwa kwa mujibu wa sheria pindi upelelezi ukikamilika na DPP kutolea maoni yake hatua inayofuata kwa mujibu wa kifungu cha 262 kifungu kidogo cha 6 ni shauri husika kufikishwa Mahakama Kuu, na kwamba hiyo ndio taarifa pekee aliyotarajia kuisikia kutoka upande wa Jamhuri Mahakamani hapo na sio kuomba hairisho

Akiwa Mahakamani hapo, Lissu ametilia shaka ukweli wa taarifa hiyo akieleza kuwa yeye hajapatiwa ‘copy’ na kwamba hana hakika kama Hakimu anayesikiliza shauri hilo amepatiwa pia, hivyo kutilia shaka kuwa huenda kinachofanywa ni Jamhuri ni sehemu ya mwendelezo unaofanywa Mahakamani hapo mara zote wa kutoa sababu ‘zisizokoma’ na iisha kuomba hairisho huku jambo ambalo yeye binafsi alionesha kutokubaliananalo

Lissu aliiomba Mahakama kutokubali maombi hayo badala yake, Mahakama itumie nafasi yake kuliondoa shauri husika Mahakamani kwakuwa upande wa Jamhuri umeonesha dalili ya kutomtendea haki mtuhumiwa ikizingatia kuwa ni siku 97 sasa yuko Mahabusu (gerezani) sambamba na wafungwa waliohukumiwa kifo

Amesema Mawakili wa serikali, DPP na wote wanaohusika na kesi hiyo kwa upande wa Jamhuri wameshindwa kukiheshimu kifungu cha 262 kifungu kidogo cha 6, na kwamba endapo Hakimu atakubaliana na maombi hayo atakuwa anafanya jambo ambalo lilikatazwa na Mahakama Kuu la kwamba katu Mahakama isiruhusu kuendeshwa na Waendesha mashtaka, kwani maombi yaliyowasilishwa na Jamhuri Mahakama Kuu yangeweza kuwasilishwa wakati shauri la msingi likiwa limeshapelekwa huko

Tundu Lissu alienda mbali zaidi, kwa kuieleza Mahakama kile alichodai kuwa kesi hiyo ni ya kisiasa na kwamba imefunguliwa kwenye mwaka wa uchaguzi, na kwamba aliyefunguliwa kesi hiyo ni kiongozi wa chama kikuu cha upinzani nchini, hivyo amedai kuwa kesi hiyo imefunguliwa ili ‘kuzima’ kampeni ya ‘No Reforms, No Election’ inayoendeshwa na chama anachokiongoza (CHADEMA)

Katika kudhihirisha msingi wa hoja yake, Lissu ameieleza Mahakama kuwa kwa sasa Wanadiplomasia, Vyombo vya Habari vya ndani na nje ya nchi na Jumuiya mbalimbali za Kitaifa na Kimataifa ikiwemo Umoja wa Ulaya (EU) na Umoja wa Mataifa (UN) kupitia kamisheni ya Haki za Binadamu imekuwa ikiifuatilia Tanzania kwa jicho ‘tofauti’ kutokana na uwepo wa shauri hilo, na kwamba kwakuwa nchi inazungumzwa ‘vibaya’ kutokana na uwepo wa shauri hilo na kwa kulinda muhimili wa Mahakama ni vyema Mahakama ikaiondoa kesi hiyo

Amesema katika kudhihirisha hilo, wakati kesi hiyo ikiendelea tayari majukwaa mbalimbali ya kimataifa ikiwemo EU, Wanadiplomasia mbalimbali wametoa maoni kwa serikali kuifuta, huku baadhi ya waangalizi wa kimataifa wakifungua shauri kwenye Mahakama ya Afrika Mashariki wakieleza kuzuiliwa kwao kuingia Tanzania kuangalia mwenendo wa shauri hilo

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kupitia kwa Hakimu Mkazi Mkuu Franco Kiswaga alieleza kukubaliana na hoja za upande wa Jamhuri, hiyo ikiwa ni baada ya kupitia vifungu na marejeo mbalimbali ya kisheria na Kikatiba hivyo kutoa hairisho la kesi hiyo hadi Julai 30 mwaka huu

Hata hivyo, Hakimu Kiswaga alitoa wito na maelekezo mahsusi kwa upande wa Jamhuri kuhakikisha ‘wanasukuma’ jambo hilo kwa haraka ili kuepusha ucheleweshwaji wa haki ya mtuhumiwa.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!