Latest Posts

ACT YAINGILIA KATI TAMISEMI KUSIMAMIA UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA, KUIBURUZA MAHAKAMANI

Na Amani Hamisi Mjege

Chama cha ACT Wazalendo kimesema hakitakwenda Dodoma kutoa maoni ya maboresho ya kanuni za uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa madai ya kuachwa kwa mambo ya msingi ya uchaguzi huo ikiwamo mamlaka itakayosimamia uchaguzi huo.

Hayo yamesemwa Jumatano Juni 12, 2024 na Katibu Mkuu wa chama cha ACT Wazalendo Ado Shaibu akizungumza na waandishi wa habari katika Makao Makuu ya chama hicho yaliyopo Dar es Salaam ambapo ameeleza kwamba hatua ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR- TAMISEMI) kutaka kusimamia uchaguzi huo ni kupoka mamlaka ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi.

“Tutakwenda Dodoma kuiamrisha TAMISEMI isimamishe mara moja hiki ambacho inaendelea kukifanya kwa sababu ni kinyume na sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, sisi ACT Wazalendo tutakwenda Dodoma kuiuliza TAMISEMI maboresho ya kanuni za kusimamia uchaguzi wa Serikali za Mitaa yatafanyika kwa mujibu wa sheria gani wakati Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ya mwaka 1979 imefutwa na Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani” Amesema Ado.

Aidha Ado amesema kwamba wanadhamiria kuishitaki TAMISEMI kwa hatua yake ya kuendeleza mchakato wa kusimamia uchaguzi huo ikiwa haitasitisha mchakato huo na kufuata sheria na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Tumekwishawasiliana na Asasi Za Kiraia (AZAKI) kuona uwezekano wa kuchukua jitihada za pamoja kufungua kesi kwa ajili ya kuzuia hatua hii inayoendelea kufanywa na TAMISEMI na ilivyo bahati tumepata mrejesho mzuri kutoka Asasi Za Kiraia ambazo zenyewe zitawaita (Wanahabari) katika wakati unaofaa kwamba maandalizi ya kufungua kesi hizo yapo tayari na hivi karibuni wametujulisha kesi hizo zitafunguliwa. Kwa msingi wa mashirikiano bora hatukuona umuhimu kama wadau wapo katika hatua za mwisho na sisi tukafungue peke yetu isipokuwa ACT Wazalendo tutatoa ushirikiano katika hatua zozote ambazo Asasi Za Kiraia ambazo itazichukua kwa ajili ya kufungua kesi dhidi ya TAMISEMI” Ameeleza Ado.

Hatua hii inajiri baada ya ACT kuwaeleza wanahabari kwamba ilipokea barua kutoka TAMISEMI ikiwaeleza kwamba TAMISEMI wanaendelea na mchakato wa maandalizi ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa na kuwaaalika ACT Wazalendo kushiriki kikao cha wadau kwa ajili ya kutoa maoni juu ya kanuni zitakazosimamia uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika mwaka huu 2024.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!