Na; mwandishi wetu
Kwa muda mrefu, Jeshi la Polisi nchini Tanzania limekuwa likituhumiwa kutumia nguvu dhidi ya raia wasiokuwa na hatia, hali inayotia shaka weledi wa maafisa wake na uhalali wa jukumu la kisheria na Kikatiba walilonalo na ulinzi wa raia na mali zao
Tuhuma hizo zimekuwa zikitolewa mara kadhaa kutoka kwa wadau mbalimbali ikiwemo wanasiasa, watetezi wa haki za binadamu, wanaharakati nk, hata hivyo ukimya unaotamalaki kutokana na ‘kelele’ hizo umekuwa ukitilia shaka kwamba huenda kile kinachofanywa ni sehemu ya utekelezaji wa maafisa wa ngazi ya juu wa Jeshi hilo, au serikali kwa ujumla wake
Alhamisi ya Aprili 25.2025, pengine inaweza kuingia miongoni mwa siku ‘ngumu’ za kukumbukwa miongoni mwa viongozi, wanachama na wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ambapo inadaiwa kuwa matumizi ya nguvu yaliyofanywa na Jeshi la Polisi dhidi ya wananchi (wengi wao wakiwa ni wafuasi wa CHADEMA) waliokuwa wamejitokeza au wako njiani kuelekea Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam kusikiliza kesi zinazomkabili Mwenyekiti wao Tundu Lissu
Katika hali isiyokuwa ya kawaida na isiyotarajiwa, kuanzia asubuhi ya siku hiyo wakazi wa hiji hilo hususani walioko kwenye barabara au maeneo ya karibu na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wameshuhudia ulinzi mkali wa maafisa wa Jeshi la Polisi wenye silaha na wasiokuwa na silaha (virungu, magari ya washawasha, Mbwa na Farasi wa Polisi wakiwemo), ikielezwa kuwa lengo ni kuzuia wafuasi wa chama hicho wasiingie kwenye viunga vya Mahakama kusikiliza kesi za kiongozi wao, katazo ambalo limewakumba pia wanahabari
Suala hilo halikuishia hapo pekee, bali imeshuhudiwa ‘vifaa’ hivyo vikitumika kisawasawa, pale ambapo maafisa hao walipokuwa ‘wakikamata’ watu kuwabeba kwenye magari yao na kuondokanao, katika wakati ambao ilifikiriwa pengine waliokamatwa wanapelekwa kwenye vituo vya Polisi kumbe hali ilikuwa tofauti, kwani inadaiwa baadhi yao ‘walitupwa’ kando au nje kabisa ya jiji la Dar es Salaam na hiyo ikiwa ni baada ya kushuhudia vipigo vikali dhidi yao
Kufuatia kadhia hiyo, Shirika la Kimataifa la Kutetea Haki za Binadamu la Amnesty International ambalo lilituma mwakilishi wake hapa nchini kufuatilia mwenendo wa kesi za Lissu, limesema linaanzisha uchunguzi rasmi dhidi ya Jeshi la Polisi la Tanzania ili kuona ni kwa namna gani limekuwa likikiuka Haki za Binadamu kwa kuwatesa raia wasiokuwa na hatia
Mapema, Ijumaa Aprili 25.2025 maafisa wa Shirika hilo wakiongozwa na Roland Ebole wamefika kwenye ofisi za makao makuu ya CHADEMA zilizopo Mikocheni, jijini Dar es Salaam na kuzungumza na viongozi waandamizi wa chama hicho wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Tanzania Bara John Heche, lakini pia wakiwa hapo wamekutana na baadhi ya majeruhi waliokumbana na kadhia ya kile kinachoelezwa kuwa ni kupigwa na maafisa wa Polisi walipokamatwa kwenye viunga vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu
Ebole amewaeleza Waandishi wa Habari kuwa shirika hilo limesikitishwa na kulaani vikali na tuhuma hizo zinazoelekezwa kwa Jeshi la Polisi kwani kiuhalisia Polisi wanapaswa kutumika kuwa wapatanishi, na wachunguzi badala ya kufanya matendo kama hayo yanayoingia moja kwa moja kwenye uvunjifu wa Haki za Binadamu na kuondoa dhana ya utawala bora kwa Taifa
Amesema Amnesty Internationali pia itachunguza madai ya uwepo wa kifo cha mtu mmoja anayetajwa kufariki Dunia baada ya kupigwa na Polisi ili kujuwa ukweli wake
Alipoulizwa endapo ziara yao hapa nchini italenga kukutana na viongozi wa vyombo vya Ulinzi na Usalama au viongozi wa serikali kwa ujumla wake, Ebole amesema kwa sasa hawafikirii kufanya hivyo kwani wanatarajia kukutana na viongozi hao pindi uchunguzi wao utakapokamilika na ripoti ya uchunguzi kutoka
Kwa upande wake, Wakili Jebra Kambole ambaye ni mwenyeji wa ugeni huo (kwa niaba ya Chama cha Wanasheria Tanganyika -TLS) amesema ziara ya wadau hao wa masuala ya Haki za Binadamu inakuja ikiwa ni sehemu ya kuonesha ushirikiano uliopo baina ya wadau wa masuala ya sheria, haki za binadamu na wanaharakati ambao mara zote wamekuwa mstari wa mbele kupigania utawala wa sheria
Amesema mara kadhaa Mawakili na Wanasheria wa Tanzania wamekuwa wakifanya ziara kwenye mataifa mbalimbali ikiwemo Kenya na Uganda kwa ajili ya kuwaunga mkono wenzao pindi wanapoona kuna viashiria vya uvunjifu wa Haki za Binadamu iwe kwa mwanataaluma mwenzao au raia wasiokuwa na hatia
Aidha, amesema kabla ya kuondoka hapa nchini maafisa hao wanatarajia kutembelea mashirika na taasisi kadhaa zilizopo hapa nchini ikiwemo LHRC, THRDC nk
Katika ziara hiyo Roland Ebole wa Amnesty International, ameambatana na Wakili kutoka Uganda Andrew Karamang, Godwin Toko kutoka Shirika la AGORA Uganda na Mjumbe wa Baraza la Uongozi wa Chama cha Wanasheria Kenya (KLS) Wakili Gloria Kimani
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wanajumuiya hao wa Afrika Mashariki (EAC) wameeleza kuwa wamelazimika kufika nchini Tanzania kufuatilia mwenendo wa kesi zinazomkabili Tundu Lissu sio tu kwa sababu ni mwanataaluma mwenzao na Rais wa zamani wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), lakini pia kuonesha kutokubaliana kwao na kile walichodai kuwa namna serikali za mataifa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki zinavyoonekana kukandamiza wapinzani wao kisiasa kwa kuwapa kesi kama ilivyo sasa kwa Tundu Lissu nchini Tanzania na Dkt. Kizza Besigye wa nchini Uganda.