Latest Posts

ASKOFU BAGONZA: WANANCHI NDIO WAMEMSHTAKI LISSU, SIO RAIS WALA POLISI

Saa chache baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kupiga marufuku urushaji wa moja kwa moja wa kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Taifa, Tundu Lissu, Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Karagwe Dkt. Benson Bagonza ameeleza kuwa hatua hiyo ni sawa na “kuwapindua wananchi.”

Katika andiko lake alilolitoa Agosti 18, 2025, Bagonza amesema kesi hiyo inamhusu siyo tu Lissu, bali wananchi wa Tanzania kwa ujumla kwa kuwa inalenga usalama wa taifa na mamlaka ya wananchi.

“Mahakama ya Hakimu Mkazi ‘imetupindua’ katika kesi inayomkabili huyo ‘mpenda madaraka’ Tundu Lissu…Sisi wananchi wa Tanzania (Jamhuri) tumeandaa mashahidi wetu ili kuhakikisha tunamtia hatiani na kumnyonga. Tuna uhakika tutamtia hatiani kwa ushahidi tulio nao,” ameandika.

Askofu Bagonza amesisitiza kuwa Lissu hashtakiwi na Rais wala Jeshi la Polisi, bali na wananchi wenyewe. Aidha, ameonya kuwa kutolewa ushahidi kwa siri na kuendesha kesi kwa siri kunaweza kuchukuliwa kama njama za kumtorosha mtuhumiwa.

“Sisi wananchi wa Tanzania (Jamhuri), kwa uzalendo tulio nao, tuko tayari kutoa ushahidi hadharani ili kila mtu ajue na hao wanaomtuma Tundu Lissu wajue kuwa tuko imara. Tundu Lissu hashtakiwi na Rais wala na Jeshi la Polisi. Anashtakiwa na sisi wananchi wa Tanzania (Jamhuri). Tunataka watu wote hasa chama cha Tundu Lissu, wajue kuwa Jamhuri yetu (wananchi) hatuna mchezo. Tutailinda nchi yetu kwa wivu mkubwa. Kesi hii iwe fundisho kwa wote wanaodiriki kuchezea mamlaka ya wananchi. Ili hili fundisho liwe kamili, kesi hii tungetamani ifanyike uwanja wa taifa. Watu waone na kusikia, na akipatikana na hatia anyongwe hadharani, siyo gerezani”.

“Kwa kuwa hata uhai wa jambazi ni muhimu utolewe kwa utaratibu, tunataka uhai wa wahaini wote utolewe kwa utaratibu na kwa uwazi. Sisi wananchi (Jamhuri) hatujamtuma yeyote kuficha chochote. Sisi ndio walalamikaji. Wananchi (Jamhuri), wana haki ya kuhisi kuwa kuna njama za kutaka kumwachia Tundu Lissu pale wanapotaka kesi iendeshwe kwa kifichoficho na ushahidi utolewe kwa siri, ipo hatari ya kuja kutuambia alitoroka!”.

“Kwa kuwa mahakama ni yetu, serikali iliyotaka kupinduliwa si kwamba ni yetu tu bali serikali hiyo ni sisi wananchi, basi tuna haki ya kuhoji maamuzi yoyote yanayoweza kutaka kumtorosha huyu mtuhumiwa asiweze kuhukumiwa ipasavyo. Kwa dalili za mahakama kutupokonya haki yetu ya kuhakikisha mhaini huyu anapata haki yake kwa uwazi, sisi wananchi (Jamhuri) tumeunda mahakama yetu ya wazi lakini iliyo vichwani mwetu, na itaendesha kesi hii na kuitolea maamuzi. Tutafungua mashtaka ya “uhaini” ya mahakama iliyotupindua. Mwenyezi Mungu asipotusikiliza (Kitu ambacho huwa hakitokei), basi tutashtaki kwa shetani”.

“Sasa wananchi wataishtaki mahakama kwa kosa la kupindua mamlaka ya wananchi. Mashahidi wetu ni wa wazi na hakimu hapokei simu ya mtu yeyote. Mahakama jiandae. Mhaini akinyongwa kwa haki, taifa linashangilia. mahakama siyo jando”.

Kauli hizo zimekuja kutokana na uamuzi wa Hakimu Mkazi Mkuu Franco Kiswaga, ambaye alisema marufuku ya urushaji wa kesi hiyo inalenga kulinda taarifa za mashahidi, na itaendelea hadi pale Mahakama hiyo au Mahakama Kuu itakapotoa amri nyingine.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!