
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima, amezitaka halmashauri zote za mkoa huo kuhakikisha zinapanga na kutekeleza mipango pamoja na bajeti zao kwa kuzingatia Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, ili kuchochea maendeleo endelevu na jumuishi kwa wananchi.
Malima ametoa kauli hiyo wakati wa kikao kazi kilichowahusisha viongozi wa Halmashauri za Wilaya za Mvomero na Gairo pamoja na viongozi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, kikao ambacho kililenga kutathmini utendaji kazi wa halmashauri za mkoa huo.
Amesema mafanikio ya maendeleo ya wananchi yanatokana na uwepo wa mipango bora inayotekelezwa kwa kuzingatia vipaumbele vya wilaya, mkoa na taifa kwa ujumla, huku akisisitiza kuwa mipango isiyolingana na dira ya taifa inaweza kusababisha matumizi yasiyo na tija ya rasilimali za umma.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa ameonesha kutoridhishwa na taarifa za utendaji kazi za Halmashauri za Wilaya za Mvomero na Gairo, na kuwataka wataalamu wa halmashauri hizo kufanya maboresho na kuwasilisha upya taarifa hizo zikiwa zimekamilika ndani ya siku nne.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro, Dkt. Mussa Ali Mussa, amewataka wakuu wa vitengo wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa kuhakikisha kila mmoja anakuwa na takwimu halisi, sahihi na zinazoeleweka katika maeneo yao ya kazi, ili kuwezesha maandalizi ya mipango mikakati ya miaka ijayo kwa ajili ya maendeleo ya wilaya hiyo.
Nao Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya za Gairo na Mvomero wameahidi kutekeleza maelekezo na maagizo yaliyotolewa na viongozi wa mkoa, pamoja na kusimamia kwa karibu maboresho yaliyoelekezwa, ikiwemo kuongeza mapato ya halmashauri na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.