Lindi.Wataalamu mbalimbali kutoka Wizara ya Uchukuzi na Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Shirika la Uwakala wa Meli (Tasac) wameunda kamati ndogo ya wataalamu kutafuta mbinu bora ya uendeshaji wa bandari ya uvuvi Kilwa.
Akizungumza katika ziara iliyoandaliwa na Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (Tasac) ya kutembelea bandari ya Kilwa leo Julai 8,2025 Mkurugenzi wa Huduma za Uchukuzi Wizara ya Uchukuzi Biseko Chiganga amesema timu hiyo ya wataalamu ikikamilisha kazi yake itatoa muelekeo ya namna ya uendeshaji wa bandari.
Biseko amesema timu hiyo ya wataalamu, imejumuisha wataalamu wa Tasac, Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA),Wizara ya Uchukuzi, Wizara ya Mifugo na Uvuvi pamoja mkoa wa Lindi.
“Tumetembelea mradi na tumefanya kikao cha pamoja kuangalia kabla ya mradi kukamilika tuangalie changamoto zilizopo na namna ya kuendesha bandari hii kwa ngazi ya wataalamu,
Yapo mambo ya kitaalamu kwa ngazi ya awali, hizi kamati za kitaalamu zikikamilisha kazi yake ndio utatoa mwelekeo wa uendeshaji wa bandari,”amesema.
Kwa upande wake Mkurugenzi Udhibiti na Usimamizi wa Huduma za Usafiri Majini Nelson Mlali amesema wametembelea kujionea ujenzi wa bandari hiyo ili kujipanga namna ya uendeshaji wake mradi utakapokamilika.
“Sisi kama wadhibiti wa usafiri wa njia ya maji tumewaeleza wadau majukumu yetu mradi utakapokamilika, mradi huu ukikamilika unakuwa bandari na bandari na bandari ni moja ya wadau unaodhibiti huduma zake kwahiyo tumeeleza namna ambavyo tutaisimamia bandari hii,”amesema.
Mlali amesema miongoni mwa majukumu yao bandari hiyo ikikamilika ni kuwapa elimu mabaharia watakaoendesha huduma za uvuvi,usimamizi wa mawakala wa meli,forodha pamoja na kampuni ndogo ndogo za kusimamia huduma za vyakula.
Akizungumzia manufaa ya mradi huo, Jackson Ally mkazi wa Kilwa Masoko amesema madereva bodaboda na vijana watakuza uchumi.
“Bandari hii kwetu tunaiona kama faraja yetu, mazao ya uvuvi yataongezeka kwasababu uvuvi utakuwa wa kisasa,tutapata ajira na vijana wengi wataondoka vijiweni,”amesema.