Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeeleza kuwa vurugu zilizojitokeza katika baadhi ya maeneo nchini hazikuathiri kwa kiwango kikubwa zoezi la kupiga kura, kwani sehemu nyingi ziliendelea na shughuli hiyo kama ilivyopangwa.
Akizungumza na wanahabari jijini Dodoma Jumatano, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM Taifa, Kenani Kihongosi, amesema vurugu zilizoonekana katika siku ya uchaguzi na siku iliyofuata zilikuwa katika maeneo machache ikilinganishwa na idadi ya vituo kote nchini.
Kihongosi ametaja mikoa ya Arusha, Dar es Salaam, Songwe na Mbeya kama maeneo ambayo vurugu zilijitokeza zaidi, baadhi zikitokea mchana wa siku ya uchaguzi, huku zingine zikiripotiwa siku ya pili. Amesema mikoa mingine nchini haikushuhudia machafuko na hivyo wananchi waliweza kupiga kura mapema bila changamoto.
Kwa mujibu wa Kihongosi, mwaka huu kulikuwa na vituo vingi zaidi vya kupigia kura kuliko wakati mwingine wowote, hatua iliyowezesha upigaji kura kukamilika mapema katika maeneo mengi. Amesema ugawaji wa vituo uliboresha mchakato, ukilinganisha na miaka iliyopita ambapo idadi ndogo ya vituo ilisababisha foleni ndefu na ucheleweshaji wa zoezi.
Kihongosi alifafanua kuwa idadi kubwa ya wananchi walipiga kura kama ilivyoshuhudiwa katika mikutano ya kampeni, akisisitiza kuwa maeneo yaliyokumbana na changamoto ni machache na hayakuathiri kwa kiasi kikubwa uhalali wa matokeo.
Aidha, amesema ushindi wa asilimia 97 ulioonekana haukufikia asilimia 100 kwa sababu katika baadhi ya maeneo wananchi walipigia vyama vingine, jambo alilosema ni sehemu ya demokrasia na uhuru wa wananchi kuchagua viongozi wanaowataka.
Aidha amesema CCM itawachukulia hatua kali viongozi wa serikali na watendaji wa umma watakaoshindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo kwani chama kimejipanga kuhakikisha maono na matarajio ya Rais Samia Suluhu Hassan yanatekelezwa kikamilifu katika ngazi zote za utawala.
Ameonya kuwa chama hakitasita kuchukua hatua kwa watendaji wazembe, viongozi wavivu au wale watakaoruhusu mianya ya rushwa, akisisitiza kuwa kila mmoja anayeshika nafasi ya uongozi analazimika kutanguliza maslahi ya Watanzania na kutimiza majukumu ya umma bila upendeleo.
Kihongosi amesema CCM itasimamia kwa karibu utekelezaji wa ahadi zote zilizotolewa wakati wa kampeni na kuhakikisha Tanzania inaendelea kupiga hatua za maendeleo kuelekea kizazi kijacho. Ameongeza kuwa chama kitaendelea kufanya kazi bega kwa bega na serikali ili kuhakikisha misingi ya upendo, amani, umoja na mshikamano inaendelea kuimarishwa.
Akizungumzia maagizo ya siku 100 yaliyotolewa na Rais Samia kwa wizara na sekta mbalimbali, Kihongosi alisema chama kinatarajia kuona utekelezaji wa maagizo hayo ukianza mara moja, akizitaka taasisi hizo “kuchakalika kwa haraka” ili kufikia matarajio ya wananchi.
Amesema kuwa CCM imeandaa vipimo maalum vitakavyotumika kupima utendaji wa kila kiongozi wa serikali. Kwa mujibu wake, viongozi watakaokosa ufanisi watakuwa wa kwanza kuondolewa, huku wale watakaoonesha uwezo na matokeo chanya wakiendelea kuungwa mkono na chama.