Latest Posts

COPRA YAIMARISHA KILIMO CHA MIKUNDE NA UFUTA, TARI YATAKIWA KUPANUA UZALISHAJI WA MBEGU

Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo, amezindua miongozo ya uzalishaji endelevu wa mazao ya ufuta, mbaazi, maharage, dengu, choroko na soya.

Akizungumza katika uzinduzi huo uliowakutanisha wataalamu wa kilimo na ushirika zaidi ya 600 kutoka mkoa wa Lindi, Chongolo amesema tukio hilo ni hatua muhimu katika kuchochea uzalishaji endelevu wenye tija na kuwawezesha wakulima kufanya kilimo cha kisasa chenye manufaa kwao.

Amesema anatambua mchango mkubwa wa COPRA katika kutekeleza wajibu wake ndani ya mageuzi makubwa ya urasimishaji wa mnyororo wa thamani wa mazao ya nafaka na mazao mchanganyiko, hatua inayolenga kutimiza sera ya kilimo-biashara nchini.

“Tumeshuhudia urasimishaji huu ukileta faida kubwa kwa wakulima, ikiwemo kuongezeka kwa kipato, kujenga mazingira ya haki,  usawa na uwazi, pamoja na usimamizi thabiti wa ubora unaokidhi vigezo vya kimataifa pamoja na ongezeko la mapato ya serikali na upatikanaji wa takwimu sahihi kwa ajili ya kupanga maendeleo.” Amesema Chongolo.

Ameipongeza COPRA kwa kuendelea kuendesha programu mbalimbali za mazao ya mikunde na ufuta, ikiwemo usambazaji wa mbegu kwa wakulima na kusema kuwa mbegu hizo bado hazitoshelezi, hivyo kuna umuhimu wa kuongeza uzalishaji na kupanua wigo ili kuhakikisha upatikanaji wa mbegu unakuwa wa kudumu.

Waziri pia ameziagiza Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) kuongeza wigo wa uzalishaji wa mbegu ili kuwawezesha wakulima kuwa na uhakika wa upatikanaji wa mbegu bora, amesema kupitia ongezeko hilo, wateja wakuu wa mbegu watakuwa Bodi ya Korosho, COPRA, Bodi ya Pamba pamoja na bodi nyingine, ili kuepusha TARI kuzalisha mbegu bila soko na kupata hasara.

Ameuhakikishia umma kuwa serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wakulima ili kuongeza uzalishaji wenye tija na kuongeza faida, kwa kuwa wakulima ndiyo msingi wa uchumi wa viwanda na ustawi wa taifa.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA), Irene Mlola, alisema kuwa miongozo iliyozinduliwa itasaidia kuongeza uzalishaji wa mazao hayo na kulinda masoko ya kimataifa.

Hata hivyo, ameainisha changamoto zinazoikabili tasnia hiyo kuwa ni pamoja na kukosekana kwa ubora na viwango kwenye ushindani wa masoko, hasa ya kimataifa; kukosekana kwa takwimu sahihi za uzalishaji na biashara; pamoja na matumizi ya pembejeo zisizo sahihi na zisizokidhi vigezo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainab Telack, amewataka maafisa ugani kushirikiana kikamilifu ili kuwawezesha wakulima kupata elimu sahihi na kuyafanya mashamba yao kuwa mashamba darasa.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!