Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro limemkamata dereva Uwimpue Bonheur (33), raia wa Rwanda na mkazi wa Kigali, aliyekuwa akiendesha gari la mizigo lenye namba za usajili RAI 878 G, aina ya HOWO, akitokea Kigali nchini Rwanda kuelekea Dar es Salaam, kwa tuhuma za kuendesha gari akiwa katika hali ya ulevi.
Kwa mujibu wa taarifa ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, SACP Alex Mkama, tukio hilo limetokea Desemba 27, 2025 asubuhi katika eneo la Kwachambo, Manispaa ya Morogoro, kando ya barabara kuu ya Morogoro–Dodoma, wakati wa operesheni za kulinda usalama wa watumiaji wa barabara.
Aidha, Kamanda Mkama amesema kuwa wakati wa kukamatwa kwa dereva huyo, kipimo cha ulevi kilionesha 171.7mg/100ml.

Jeshi la Polisi limeeleza kuwa mtuhumiwa huyo amezuiliwa kuendesha chombo hicho kwa usalama wake na wa watumiaji wengine wa barabara, huku taratibu na hatua nyingine za kisheria zikiendelea.
Katika hatua nyingine Jeshi hilo linamshikilia mwanaume mmoja aitwaye Rashid Hussein Paulo (35), mkulima na mkazi wa Msowelo, kwa tuhuma za kumuua Steven Elia Mayungu (26), mkulima na mkazi wa Mayungu, kufuatia ugomvi uliodaiwa kutokea kati yao.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Desemba 27, 2025 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, SACP Alex Mkama, tukio hilo lilitokea Desemba 26, 2025 majira ya saa tano usiku katika kitongoji cha Shuleni, kijiji na kata ya Lumuma, wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro. Inaelezwa kuwa katika tukio hilo, marehemu alipata majeraha makubwa baada ya kushambuliwa kwa chombo chenye ncha kali katika eneo la kifua.
Akizungumza kuhusu chanzo cha tukio hilo, Kamanda Mkama amesema uchunguzi wa awali umeonyesha kuwa ugomvi huo ulitokana na wivu wa mapenzi, ambapo mtuhumiwa alidai kuwa marehemu alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na mke wake.
Jeshi la Polisi limeeleza kuwa mtuhumiwa anaendelea kushikiliwa kwa ajili ya kukamilisha taratibu na hatua zaidi za kisheria.