Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amezipongeza na kuahidi ushirikiano kwa asasi za kiraia (NGOs) kutokana na mchango wao mkubwa katika maendeleo ya kiuchumi, kijamii, na utawala bora nchini.
Dkt. Biteko amesema hayo leo Septemba 6, 2024 jijini Dodoma wakati akihutubia Mkutano wa Jukwaa la Mwaka la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali.
“Serikali haitapuuza mchango wenu, kwani asasi za kiraia ni wadau muhimu wanaosaidia kufikia malengo ya maendeleo.” Aliongeza kuwa zaidi ya mashirika 9,777 yanasajiliwa nchini, yakilenga kutoa huduma bora kwa Watanzania”, amesema Dkt. Biteko.
Kwa mujibu wa Dkt. Biteko, mashirika yasiyo ya kiserikali yamekuwa na mchango mkubwa siyo tu katika nyanja za kijamii na kiuchumi, bali pia katika utawala bora. Aliendelea kwa kusema kuwa mashirika hayo yameajiri watu zaidi ya 21,000 na kuchangia kiasi cha shilingi trilioni 2.6 kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali. Hivyo, alisisitiza kuwa serikali itashirikiana kwa karibu na mashirika hayo badala ya kuyaona kama wapinzani.
Akitaja baadhi ya faida zilizotokana na ushirikiano na asasi za kiraia, Dkt. Biteko alisema kuwa mashirika hayo yamechangia jitihada za kuwaletea wananchi maendeleo kupitia miradi mbalimbali katika sekta kama afya, kilimo, elimu, na maji.
“Kwa mfano, katika sekta ya afya, mashirika haya yamekuwa yakifanya kazi kubwa ya kusaidia serikali kuwahudumia Watanzania kwa upendo, jambo linalowafanya wananchi kufurahia huduma zinazotolewa,” alisema.
Aidha, alielezea hatua ambazo serikali imezichukua kuboresha mazingira ya utendaji kazi wa mashirika hayo, ikiwa ni pamoja na kuandaa Mwongozo wa Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (2020) na Mfumo wa Kielektroniki wa Usajili na Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali.
Pia alieleza kuwa Kitabu cha Mchango wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali katika Maendeleo ya Taifa, na Ramani ya Kidigitali ya Utambuzi wa Mashirika hayo ni miongoni mwa hatua za serikali kusaidia mashirika yasiyo ya kiserikali kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.
Dkt. Biteko pia alizungumzia mkakati wa uanzishwaji wa Mfuko wa Pamoja wa Ruzuku kwa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, ambao alisema utawezesha mashirika hayo kupata fedha bila masharti magumu ya ufadhili.
“Mfuko huu utawezesha mashirika kupata fedha za kutekeleza miradi yao kwa ufanisi zaidi, jambo linalosaidia maendeleo ya taifa letu,” alisema.
Wakati akihitimisha hotuba yake, Dkt. Biteko alitoa rai kwa mashirika hayo kuendelea kuwa mfano wa maadili ya Kitanzania na kuhakikisha fedha wanazozipata kutoka kwa wafadhili zinatumika kwa kazi zilizokusudiwa.
“Tunatarajia kuona mashirika haya yakiheshimu maadili ya Kitanzania na kutumia fedha kwa ajili ya malengo yaliyokusudiwa, ikiwa ni pamoja na kuchangia maendeleo ya jamii,” alisema.
Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko alielezea umuhimu wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia akikumbusha kwamba serikali imejipanga kuhakikisha kwamba asilimia 80 ya Watanzania watatumia nishati safi ifikapo mwaka 2034 ili kupunguza idadi ya vifo vinavyosababishwa na matumizi ya nishati isiyo salama.
Naye Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima, alisema kuwa mashirika yasiyo ya kiserikali yameendelea kufanya kazi nzuri nchini, na Wizara yake itaendelea kuweka mazingira bora ili mashirika hayo yaendelee kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.
Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, Bw. Jasper Makala, alisema sekta ya mashirika yasiyo ya kiserikali imeendelea kukua mwaka hadi mwaka na kuahidi kuendelea kushirikiana na serikali katika kufanikisha malengo ya maendeleo ya taifa.