Kampuni ya GF Trucks & Equipment Ltd imeibuka mshindi wa jumla wa Maonesho ya Biashara ya Kimataifa Sabasaba kwa mwaka 2025, kupitia kiwanda chake cha kuunganisha magari makubwa, GF Vehicle Assemblers (GFA) kilichopo Kibaha, mkoani Pwani.
Maonesho hayo yaliyofunguliwa rasmi Juni 28, yameshirikisha zaidi ya kampuni 3,000 kutoka ndani na nje ya nchi, zikiwemo kutoka China, Korea Kusini, Uturuki, Ulaya na nchi mbalimbali za Afrika.
Mgeni rasmi katika ufunguzi na utoaji wa tuzo alikuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ambaye alipata fursa ya kutembelea mabanda ya maonesho, likiwemo banda la GF Trucks & Equipment.

Rais Mwinyi alijionea bidhaa mbalimbali zinazotolewa na kampuni hiyo, ikiwemo magari madogo ya Hyundai na Mahindra, pamoja na magari makubwa ya mizigo ya FAW, mitambo na mashine nzito za XCMG. Alielezwa pia kuhusu mchakato wa kiufundi wa uunganishaji wa magari katika kiwanda cha GFA — kiwanda cha kwanza cha aina yake nchini Tanzania.
Pia Mwinyi aliwapongeza GF kwa kuibuka kuwa vinara wa ma maonesho hayo na kuwataka wasibweteke, isipokuwa wapanue Zaidi uwekezaji mpaka Zanzibar.
Akizungumza mara baada ya kupokea Tuzo ya Ushindi wa Jumla, Mkurugenzi wa GF Trucks & Equipment, Ali Karmali, amesema ushindi huo ni matokeo ya kujitolea kwa wafanyakazi wao na mazingira bora ya uwekezaji yaliyowekwa na Serikali.

“Tunajivunia kuwa kampuni ya kwanza Tanzania kuanzisha kiwanda cha kuunganisha magari. Tupo katika awamu ya tatu ya upanuzi wa GFA ambayo itazalisha ajira zaidi ya 3,000 kwa Watanzania,” alisema Karmali.
Aliongeza kuwa ushindi huo si wao pekee, bali ni wa Watanzania wote wanaonufaika na ajira, ujuzi na huduma bora za bidhaa zinazozalishwa nchini.
GF Trucks & Equipment inaongoza kwa uuzaji wa magari mazito aina ya FAW, mitambo ya barabara na madini ya XCMG, pamoja na magari ya abiria na kibiashara ya Hyundai na Mahindra.