Kampuni ya GF Trucks & Equipment Ltd, iliyotwaa ushindi wa jumla katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam, imeadhimisha ushindi huo kwa staili ya kipekee kwa kuwajumuisha wadau wake wakuu — wafanyakazi, wateja na washirika wa karibu — katika viwanja vya Sabasaba.
Katika hafla hiyo ya shukrani na furaha, GF Trucks iliweka wazi kuwa mafanikio yao hayakutokea kwa bahati, bali ni matokeo ya mshikamano wa “Utatu” baina ya Uongozi, Wafanyakazi, na Serikali, kama alivyosema Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa GF, Mehboob Karmali.
“Serikali imeweka mazingira mazuri kwa wawekezaji, sisi tukajenga msingi wa ushirikiano baina ya uongozi, wafanyakazi wetu na wateja. Huu ndio utatu wa mafanikio yetu,” alisema Karmali.
Kampuni hiyo, ambayo inauza magari ya kila aina – kutoka magari madogo ya matumizi binafsi hadi makubwa ya migodini na kilimo – inajivunia kuwa na kiwanda chake cha kuunganisha magari, GF Vehicle Assemblers (GFA) kilichopo Kibaha, mkoani Pwani.
Meneja wa Kiwanda cha GFA, Ezra Mereng, alisema ushindi huo ni matokeo ya kazi ya pamoja na uongozi bora. Aliongeza kuwa kupitia sera na mazingira wezeshi ya Serikali kwa wawekezaji, sekta ya magari inatarajiwa kuwa miongoni mwa maeneo yatakayochangia kwa kiasi kikubwa pato la taifa.
“Tunapambana kuhakikisha bidhaa kutoka Tanzania zinaaminika sokoni. Huu ni mwanzo tu — tutafika mbali,” alisema Mereng.
Bidhaa zinazouzwa na GF Trucks ni pamoja na magari ya chapa za FAW, XCMG, Mahindra, na Hyundai, pamoja na mitambo mizito ya kilimo, ujenzi na uchimbaji madini.
Ushindi huu umetajwa kuwa si tu heshima kwa kampuni, bali pia ni kielelezo cha mchango mkubwa wa sekta binafsi katika uchumi wa taifa.