Latest Posts

HALMASHAURI YA WILAYA YA SHINYANGA YAKAMILISHA JENGO LAKE KWA BILIONI TATU

Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga imetangaza mabadiliko makubwa katika utoaji wa huduma kwa jamii kufuatia kukamilika kwa jengo lake jipya la utawala lililogharimu shilingi bilioni tatu. Jengo hilo, ambalo limeanza kutumika rasmi tangu Aprili 16, 2025, limetajwa kuwa muarobaini wa changamoto ya ufinyu wa nafasi uliokuwa ukiwakabili watumishi na wananchi kwa kipindi kirefu.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Bi. Kalekwa Kasanga, akielezea mafanikio hayo amebainisha kuwa tangu kuanzishwa kwake, halmashauri hiyo ilikuwa ikihudumia wananchi kutokea Manispaa ya Shinyanga, hali iliyokuwa ikiwalazimu wananchi kufuata huduma nje ya maeneo yao ya kiutawala. Hata hivyo, kufuatia maelekezo ya Serikali ya mwaka 2019, halmashauri ilihamia kijiji cha Isilamagazi ikitumia ofisi za muda za taasisi ya World Vision, kabla ya Rais Samia Suluhu Hassan kuwezesha upatikanaji wa fedha za ujenzi wa jengo la kudumu kuanzia mwaka 2021.

Akizungumzia ufanisi wa jengo hilo jipya, Bi. Kasanga amesisitiza: “Kwa dhati kabisa tunamshukuru Rais wetu Samia Suluhu Hassan kwa kutuwezesha kupata jengo hili kubwa ambalo lina ofisi nyingi za kutosha na linatumika na wafanyakazi wote 130 wa halmashauri kutoka idara 20. Utendaji kazi umeboreka kwa sababu hakuna kubanana tena.”

Upatikanaji wa ofisi hizo sasa unatoa fursa kwa halmashauri hiyo kuratibu na kuhudumia watumishi wengine 2,450 walioko kwenye vituo vya afya, zahanati, na shule katika kata zote 26 za wilaya hiyo. Bi. Kasanga ameweka wazi kuwa mazingira bora ya kazi ni kichocheo cha ufanisi:

 

“Mtu yeyote ili afanye kazi lazima awe kwenye mazingira mazuri, kwa hiyo jengo hili ni miongoni mwa hatua zilizochukuliwa na serikali kujenga mazingira wezeshi ili kuweza kutoa huduma bora kwa wananchi.”

Sambamba na mafanikio hayo ya kiutawala, Mkurugenzi huyo amemshukuru Rais kwa ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Amali ya Mwambasha. Mradi huu unatajwa kuwa wa kipekee mkoani Shinyanga kwani unalenga kutoa elimu ya vitendo (technical skills), jambo ambalo litaandaa vijana wa wilaya hiyo kuwa na ujuzi wa kujiajiri na kuendana na mahitaji ya soko la viwanda.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!