Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Bara, John Heche, amesema ni sehemu ya mipango ya chama hicho kuhakikisha wazee wote nchini wenye umri wa kuanzia miaka 60 wanapata pensheni ya Serikali kama njia ya kutambua mchango wao katika ujenzi wa Taifa.
Akizungumza Oktoba 1, 2025 katika mkutano wa mtandaoni uliofanyika kwa heshima ya maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani, Heche amesema mpango huo ni wa kidemokrasia na kijamii, wenye lengo la kuondoa dhuluma na upungufu wa hifadhi ya jamii unaowakabili wazee wengi.
“Hili taifa halijengwi na watumishi wa umma pekee, linajengwa na Watanzania wote. Ndiyo maana CHADEMA tukasema kila anayetimiza miaka 60 tutampa pensheni ya Serikali,” amesema Heche.
Heche ameongeza kuwa karibu asilimia 40 ya mapato ya Serikali hupotea kutokana na ufisadi na rushwa, kwa mujibu wa ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
“Upotevu huu ndio unaosababisha makundi muhimu kama wazee kukosa fedha zao za msingi,” amesema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Wazee CHADEMA, Susan Lyimo, amesema matamanio na ustawi wa wazee nchini yameendelea kudidimia kutokana na kile alichokiita “demokrasia duni na chaguzi zisizo huru na za haki”.
Amesema hali hiyo imewaweka wazee wengi nje ya mifumo ya hifadhi ya jamii. “Ni asilimia 7 pekee ya wazee nchini walio kwenye hifadhi ya jamii, huku asilimia 93 wakiwa nje ya hifadhi. Hii ni hali mbaya kwa taifa letu,” amesema Lyimo.
Katika salamu zilizotolewa na wazee kutoka maeneo mbalimbali, wamesema kuna haja ya Serikali kuhakikisha kundi la wazee linapata uwakilishi wake Bungeni sawa na makundi mengine ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu.
“Imefika mahali sasa wazee tumesahaulika. Vijana, walemavu na akinamama wanawakilishwa bungeni, na sisi wazee tunataka uwakilishi wetu,” amesema mmoja wa wazee.
Aidha, wazee wamependekeza kuanzishwa kwa Wizara maalumu ya kushughulikia masuala ya wazee, wakisema hatua hiyo itawawezesha kushiriki moja kwa moja katika mijadala ya maendeleo na sera.
Maadhimisho ya mwaka huu kwa CHADEMA yamebebwa na kaulimbiu: “Demokrasia duni na uchaguzi usio wa haki, athari zake kwa matamanio, ustawi na haki za wazee.”