Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC) kimeitambulisha kwa Umma ilani yake ya uchaguzi ya mwaka 2025 ikiwa na vipaumbele kadhaa vyenye lengo la kuhakikisha huduma za kijamii na kiuchumi zinapatikana kwa usawa na bila ubaguzi kwa wananchi wote.
Akizungumza Agosti 11, 2025 mkoani Dar es Salaam wakati wa kuitambulisha ilani ya uchaguzi ya chama chao, Mwenyekiti wa Alliance for Democratic Change (ADC), Shaban Itutu, amesema: “Ilani ya ADC ni ilani ya wananchi. Kura yako ni sauti yako, na ilani ya ADC inavyosema, tunataka kila mwananchi apate huduma bora za elimu na afya bure, mikopo bila riba, na haki sawa katika sekta zote za maisha. Ilani hii si ya chama tu, ni ya watu wote. Ni ahadi yetu kwa Taifa.”
ADC imeahidi kutoa elimu bure kuanzia mtoto anapozaliwa hadi kumaliza masomo, pamoja na huduma za afya bure maisha yake yote. Pia, chama kimepiga marufuku vizuizi vya kutoa huduma kwa maiti ili familia zipate heshima na faraja bila gharama zisizo za lazima.
Chama kimependekeza mfumo wa elimu mbadala ambapo mwanafunzi atakapomaliza darasa la saba ataelekezwa kwenye mafunzo ya ufundi stadi ili kumpa ujuzi wa moja kwa moja wa kujipatia kipato hii ni kwasababu ya elimu ya sasa kutotoa fursa ya kujiajiri na kuchukua muda mrefu wa vijana kukaa masomoni.
Akizungumzia mfumo wa afya, Itutu amesema Ilani ya chama chao itatekeleza huduma ya afya kuwa bure akitoa mfano imekuwa na mfumo wa huduma ya afya bure kwa wananchi wote ambapo wananchi hupata matibabu bure na wagonjwa wenye maradhi makubwa husafirishwa kwenda nje ya nchi kwa gharama za Serikali.
ADC imeahidi kuondoa kodi kwa vifaa vya wavuvi na kutotoza ada yoyote kwa mitumbwi, huku mazao yatakayopatikana baada ya kuvua yakitozwa gharama ndogo zilizopangwa. Aidha, ADC kimepanga kuwapatia wavuvi meri za kisasa za uvuvi ili kuongeza tija na mapato katika sekta hiyo.
ADC imependekeza mageuzi ya umri wa kustaafu, ambapo mtu atastaafu rasmi akifikisha miaka 70, ikielezwa kuwa watu wengi wanastaafu wakiwa bado na nguvu na uwezo wa kufanya kazi. Hata hivyo, Itutu amesema serikali ya ADC itaangalia kwa umakini kada muhimu ambazo zina wataalamu wachache au zinazohitaji ujuzi maalum kama vile madaktari bingwa, watafiti na wahandisi wa kiwango cha juu ili kuendeleza ajira zao kwa muda mrefu zaidi kadri inavyohitajika kwa maslahi ya taifa.