Katibu wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Kilimanjaro (MECKI), Devis Minja, ametoa wito kwa Serikali, kuanzisha sheria itakayowataka wananchi kupanda miti kulingana na umri wa marehemu wakati wa mazishi, pamoja na wale wanaosherehekea siku zao za kuzaliwa kupanda miti kwa idadi inayolingana na umri wao.
Minja amesema hatua hiyo itasaidia kuunganisha maisha ya mwanadamu na ustawi wa mazingira kwa njia ya heshima, kumbukumbu na uhai mpya kwa vizazi vijavyo.
Ametoa ushauri huo wakati akiongoza Wanahabari wa Mkoa wa Kilimanjaro katika zoezi la upandaji miti 300 rafiki wa mizingira na matunda katika Shule ya Sekondari Mtakuja Wilayani Moshi Mkoani Kilimanjaro na kusema wazo hilo linaweza kuwa chachu ya mabadiliko ya kimazingira iwapo litaungwa mkono na sera za kitaifa, likiambatana na elimu endelevu kuhusu mabadiliko ya tabianchi.
“Kwa mfano ,mtoto mwenye miaka 10 anaposherehekea kuzaliwa kwake,apande miti 10 kwa kushirikiana na familia, shule au Jamii,vivyo hivyo,kwa mtu aliyefariki,ndugu na jamaa zake wapande miti idadi ya miaka aliyokuwa nayo Marehemu kabla ya kuzika na waionesha kwa mamlaka,mfumo huu utahusisha Jamii Moja kwa moja katika ulinzi wa mazingira kwa njia ya kihisia na heshima kwa maisha ya binadamu” alisema Minja.
Aidha, amesema iwapo Wizara ya Mazingira itaandaa mwongozo rasmi wa utekelezaji na kushirikiana na mamlaka za serikali za mitaa, taasisi za dini na familia, litakuwa jambo lenye athari chanya kwa jamii kwa kuongeza uelewa wa misingi ya utunzaji mazingira kwa vitendo. “Ni wakati sasa taifa letu litazame upya namna ya kuunganisha maisha ya binadamu na mazingira kwa vitendo vinavyogusa kila mtu moja kwa moja,” alisema Minja.
Katibu huyo pia ametoa wito kwa mashirika ya kimataifa kuunga mkono jitihada hizo kupitia programu za kijamii na miradi ya upandaji miti kwenye maeneo ya shule, hospitali, na jamii zilizoathirika na uharibifu wa mazingira kwani kwa kufanya hivyo kila mtu atapanda angalau mti mmoja kila mwaka kwa tukio muhimu la maisha, taifa linaweza kufikia malengo ya kuongeza uoto wa asili na kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi kwa mafanikio.
Kwa upande wao Wanafunzi wa shule hiyo wameshukuru Klabu ya Wanahabari Kilimanjaro kwa kuwatembelea na kupanda miti na kuahidi kuitunza kutokana na shule hiyo kuwa mpya yenye kuhitaji mazingira mazuri ya kujisomea nje ya darasani.